AUWSA YAJIPANGA KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI SAFI

 

📌SALMA HAROUN & JOSEPHINE MTWEVE

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) imetenga shilingi Bilioni 11.8 kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Justine Rujomba wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, amesema mahitaji halisi kwa sasa ni lita 124,789,000 kwa siku, Jiji la Arusha  lita 109,689,250 na lita 15,099,750 katika miji midogo.

Amesema kwa sasa maji yanayozalishwa ni lita 84,500,000 kwa siku kutoka kwenye vyanzo vya visima virefu, chemchem na mito sawa na asilimia 68% ya mahitaji.

Kabla ya uwekezaji serikali kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa, uzalishaji wa maji ulikua wastani wa lita 48,000,000 kwa siku na huduma ya uondoaji wa maji taka ulikuwa asilimia 7.6% ya wakazi wa Jiji la Arusha

Aidha Mhandisi Rujomba amesema serikali kupitia fedha za mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya maendeleo ya Afrika (AFDB) imeweza kuwekeza katika kuboresha hali ya upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Arusha.

Hata hivyo amesema AUWSA imejipanga kutekeleza miradi ya Maji Safi kwa ufanisi na kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wa Arusha wanapata huduma ya Maji Safi na salama kwa asilimia 95% mjini.

AUWSA imewaasa wananchi wa Arusha kuendelea kutunza miundombinu pamoja na vyanzo vya maji, kulipia ankara kwa wakati na kushiriki katika kusaidia kuzuia wizi wa maji kwa kuwafichua wanaohusika na wizi huo.

 

Post a Comment

0 Comments