TMDA YAKAMATA DAWA NA VIFAA TIBA AMBAVYO HAVIJASAJILIWA VYENYE THAMANI YA SH MILLIONI 350

 

📌RHODA SIMBA

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata aina mbalimbali za dawa zikiwemo za serikali, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 350 katika operesheni maalum iliyofanyika katika mikoa 14 hapa nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo akizungumza jijini Dodoma amesema operesheni hizo tatu zilizofanyika kwenye maeneo 1,355 ya biashara zimewezesha kukamatwa kwa aina 4 za dawa bandia, aina tano za dawa duni dawa za Serikali na dawa ambazo hazijasajiliwa, huku thamani ya dawa na vifaa tiba vya Serikali ikifikia shilingi milioni 13.

Thamani ya dawa na vifaa tiba vya Serikali ilikuwa ni shilingi 13,035,000 na thamani ya dawa zilizokwisha muda wa matumizi ilikuwa ni shilingi 28,642,150, hatua za kisheria zilichukuliwa dhidi ya watuhumiwa. Hata hivyo kiasi cha bidhaa duni na bandia katika soko limekuwa kikipingua ambapo hadi sasa tatizo la dawa duni na bandia liko kwa asilimia 1.

Akielezea mpango mkakati wa kitaifa wa miaka mitano 2021 hadi 2026 wa kupambana na tumbaku pamoja na mpango kazi wa miaka mitano wa udhibiti wa tumbaku, Mkurugenzi mkuu huyo wa TMDA amesema mfumo wa udhibiti wa bidhaa 51 za tumbaku zilizoko kwenye soko tayari zimetambuliwa:

Aidha, amesema kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2022 jumla ya viwanda 17 vya dawa 26 vya vifaa tiba na 6 gesi tiba vimesajiliwa na kuanza kufanya kazi.

Viwanda 15 vya dawa ambavyo 8 vimesajiliwa na 7 vipya ndani ya Nchi vilikaguliwa ambapo viwanda 2 Kati ya 7 vipya vimekidhi vigezo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni,hili ni ongezeko la viwanda 6 sawa na asilimia  67 ukilinganishwa na viwanda 9 vilivyokaguliwa mwaka 2020/21.

Moja ya majukumu ya TMDA ni pamoja na kusajili bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Katika kipindi cha mwaka 2021/2022, mamlaka hiyo imesajili jumla ya bidhaa 1,286 ambapo kati yake bidhaa za dawa za binadamu na mifugo ni 933 huku vifaa tiba na vitendanishi vikiwa ni 353 na hivyo kufanya idadi ya bidhaa zilizosajiliwa kufikia 8,831 hadi sasa.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments