📌JAMES K. MWANAMYOTO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inajenga wodi ya afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya Kibena iliyopo wilayani Njombe itakayoboresha huduma ya afya ya uzazi kwa akina mama ikiwa ni pamoja na kutunza watoto waliozaliwa kabla ya muda mkoani Njombe.
Jengo hili tulilolikagua leo ni wodi ya akina mama wanaojifungua, vilevile jengo hili limeandaliwa pia kwa ajili ya matunzo ya watoto ambao wamezaliwa kabla ya muda maalum kama watoto njiti
Mhe. Jenista
Akizungumzia idadi ya miradi ya TASAF mkoani Njombe, Mhe. Jenista amesema, Mkoa wa Njombe una miradi 54 ambayo imegawanyika katika halmashauri zote, na kuongeza kuwa, jambo la kufurahia ni kuwa miradi hiyo imelenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Halmashauri za Wilaya ya Njombe, Makambako na Makete zilikuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa madarasa katika shule za msingi na kuna maeneo yalikuwa na shule shikizi hivyo kuwalazimu watoto wa shule kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kuhudhuria masomo, lakini Serikali kupitia maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya utekelezaji wa miradi ya TASAF imefanikiwa kutatua changamoto zote hizo
Mhe. Jenista
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Kissa Kasongwa amesema kuwa jengo hilo la afya ya mama na mtoto ambalo litatumika pia kuhifadhi watoto wanaozaliwa kabla ya muda litatatua changamoto kubwa ya huduma hiyo iliyokuwa ikiwakabili wananchi katika wilaya yake.
Wananchi wilayani Njombe waliposikia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia TASAF ametoa shilingi milioni 92 kujenga jengo hili la afya ya uzazi kwa akina mama, nao walichangia shilingi milioni 11 ndani ya wiki moja ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais za kuboresha huduma katika sekta ya afya
Mhe. Kasongwa
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bi. Sharifa Nabarang’anya amesema, wananchi wake wanamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwenye sekta ya afya, elimu na miundombinu, akiainisha kuwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu, halmashauri yake imepokea jumla ya shilingi milioni 495 kwa ajili ya kujenga zahanati tatu ambazo zitakamilika tarehe 30 Agosti, 2022 na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bi. Kuruthum Sadick amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi mikubwa inayoboresha huduma za kijamii kwa wananchi, hususan mradi wa ujenzi wa jengo la afya ya mama na mtoto ambao utatoa huduma kwa akina mama wengi wa Mkoa wa Njombe.Akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. John Steven ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi TASAF amesema kuwa, ameambatana na Waziri Jenista Mhagama kwa ajili ya kukagua miradi ya TASAF inayofadhiliwa na Shirika la Uzalishaji Mafuta Duniani (OPEC) ambayo itatekelezwa mpaka mwaka 2025 mkoani Njombe.
Jumla ya miradi 54 ya TASAF mkoani Njombe inafadhiliwa na Shirika la Uzalishaji Mafuta Duniani (OPEC).
0 Comments