📌RHODA SIMBA
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo ameutaka uongozi wa Jiji la Dodoma kufunga mifumo ya gesi asilia katika soko kubwa la mfano la wamachinga linalojengwa hapa ili kuzuia uchafuzi wa mazingira katika eneo hilo litakalokua na mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara na wateja.
Dkt. Jafo amesema hayo leo Julai 26 jijini hapa alipotembelea soko jipya la machinga ambapo amesema kuwa kwa upande wa kimazingira hatua waliofikia inaridhisha lakini ni muhimu kuwa na mfumo mmoja wa mitungi ya gesi kupitia gesi asilia.
Tunapokwenda huko baadae ile mitungi ya gesi tunatakiwa tuwe na mfumo mmoja hapa tuwaambie TPDC waje kuweka tenki moja kubwa ambalo lile litakuwa na gesi asilia watu wawe wanatumia kuweka mfumo wa kulipa bill kwa mabomba na kufungiwa mita hii itakuwa ni njia salama kuliko kila mmoja kuja na mtungi wake
Dkt.Jafo.
Waziri Jafo amesema Mpango wa Serikali ni kuhakikisha Nishati inayotumika ni Nishati kubwa ya gesi na kutokana na hilo ni muhimu soko hilo liwe na mfumo huo mkubwa wa gesi asilia.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amesema kuwa mradi huo ni wa machinga wa Jiji hilo na wamejitahidi kuhakikisha kuwa kila machinga ananufaika na soko hilo.
Amesema katika soko hilo limelenga kuwanufaisha wamachinga walio na mitaji midogo na lengo ni kumtoa alipo sasa ambapo mazingira yake sio rafiki na ikiwezekana atoke kuwa machinga mdogo mpaka afikie kuwa na mtaji mkubwa.
Humu hamna mtu wa Serikali mwenye kibanda tunataka mtu mwenye mtaji wa kuanzia fungu la nyanya la miatano, mkaa fungu moja ili apike chakula auze huko ambako anauza chini ya turubai tunataka huyu mtu aje apike hapa kwenye gesi
Tunataka atoke kwenye kupika kilo moja kwa siku afike kwenye kupika kilo 25 kwa siku ili aje awe anatoa ushahidi kwamba mimi nilianzia kwenye lile soko hapo na sisi ndipo tutasema huyu mtu tumemfanikisha sisi,"alisema Mkuu wa mkoa.
Naye Afisa Mazingira Jiji la Dodoma Dikson Kimaro amesema kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri watahakikisha wanayasimamia na kuyatekeleza ikiwemo kuongeza miundombinu ya uvunaji wa maji mvua.
Mohamed Building ambaye ndiye mkandarasi amesema kuwa anaishukuru Serikali ya awamu ya 6 kwa kuweza kuwapa kipaumbele hasa wakandarasi Wazawa na kuahidi kuboresha yale maeneo waliyoelekezwa.
Amesema ikiwa hilo ndilo soko la kisasa la machinga kwa Tanzania watahakikisha linakuwa na hadhi yake na kuendelea kuipa heshima makao makuu ya Nchi.
0 Comments