📌RHODA SIMBA
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema jumla ya watoto milioni 12,132,049 wamefanikiwa kupata chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio ambapo ni sawa na asilimia 117.8 ya malengo ya Serikali waliyojiwekea.
Aidha amesema kampeni hiyo ililenga kuwapatia chanjo watoto milioni 10,295,316 kwa Tanzania bara, ambapo ufanisi wa utoaji wa chanjo hiyo umetofautiana kutoka Mkoa mmoja hadi Mkoa mwingine.
Ameyasema hayo leo June Mosi jijini hapa wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu kampeni ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio kwa watoto wa chini ya miaka mitano iliyofanyika nchini kuanzia mei 18 hadi mei 21.
“Haya ni mafanikio makubwa kwetu sote, napenda kutoa pongezi kwa viongozi wakiwemo waheshimiwa wakuu wa Mikoa na Wilaya, Timu za Uendeshaji wa huduma za afya ngazi ya Mikoa na Halmashauri, watumishi wa afya pamoja na wadau mbalimbali wakiwamo wadau wa maendeleo kwa kusimamia kikamilifu maandalizi, uzinduzi na utekelezaji wa kampeni katika maeneo yao kwa umahiri mkubwa”
“Nitumie fursa hii, kutoa wito kwa Viongozi wa ngazi mbalimbali, Wadau wa Maendeleo, wataalamu wa afya, wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa kampeni zinazofuata ambazo zinatarajiwa kufanyika mwezi Julai na Agosti, 2022 kwa tarehe ambazo zitatangazwa baadaye”.amesema Ummy
Amesema kila mwananchi anayo sababu ya kuilinda nchi na watoto dhidi ya ugonjwa wa Polio na kila Mzazi/Mlezi ahakikishe watoto wanapata chanjo ya Polio.
“Bado tunaweza kutunza rekodi ya Tanzania kuwa nchi ya Tanzania ni nchi isiyokuwa na ugonjwa wa Polio duniani na natoa wito kwa wananchi kuendelea kuwapeleka watoto wote kupata chanjo dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za chanjo nchini” amesema Ummy
Sambamba na hayo amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Afya imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tishio la mlipuko wa ugonjwa wa Polio hapa nchini.
Virusi vya Polio vinapoingia mwilini huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha madhara kiafya ikiwa ni pamoja na kupooza kwa ghafla kwa kiungo au viungo na hata kupelekea kifo
“Dalili za awali za ugonjwa wa Polio ni pamoja na homa, uchovu, maumivu ya kichwa, kutapika, kukakamaa shingo na maumivu ya viungo. Ugonjwa wa Polio hauna tiba. Njia kuu ya kuzuia ugonjwa huu ni kuwapatia chanjo ya polio watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano”Amesema
Kadhaika amesema kampeni hii inatakiwa kufanyika kila baada ya wiki nne, ili kuhakikisha watoto wote walengwa wanafikiwa, na mkakati wa kuchanja watoto wote katika vituo vya kutolea huduma pamoja na kuwafuata walipo yaani nyumba kwa nyumba kwa kutumia huduma mkoba na tembezi hutumika.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 18 Mei, 2022, Wizara ya Afya ilizindua awamu ya pili ya kampeni ya Kitaifa ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio hapa nchini,na katika zoezi hilo mkoa wa Ruvuma iliongoza kwa kuvuka lengo kutoa chanjo kwa 131% ikifuatiwa na Shinyanga 128% na Rukwa 123%.
Mikoa mingine ni Pwani 122%, Arusha 122%, Mbeya, Geita, Dar es Salaam na Simiyu yote ina 121%, Singida, Dodoma na Tabora 118% , Kigoma, Njombe, Katavi 117%, Morogoro 116%, Mara, Mtwara, Lindi na Tanga 115%, Kilimanjaro na Mwanza 114%, Manyara na Iringa 113%, Songwe na Kagera 111%.
0 Comments