📌RHODA SIMBA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itakuwa karibu na wahandisi kwa kuwapatia miradi midogo na mikubwa inayokuja ili kuendelea kuiheshimisha nchi.
Rais Samia ameyasema hayo kwa njia ya simu katika kongamano la wahandisi na makandarasi lililokuwa na lengo kumpongeza lililofanyika jijini Dodoma
Nawaahidi Serikali itakuwa karibu na wahandisi na kuhakikisha katika miradi midogo na mikubwa inayokuja mtapata nafasi nyingi ya kufanya kazi kama makandarasi wazawa hii itatupa heshima ya kuendelea kuitangaza nchi yetu.
Niseme tu mjipange vizuri kufanya kazi kuna miradi mikubwa inakuja hivi karibuni nitahakikisha mnapata nafasi ya kuifanya
Rais Samia.
Awali akizungumza na makandarasi na wahandisi wa miundombinu Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya aliyekuwepo katika kongamano hilo amesema Serikali itahakikisha inawajengea uwezo wakandarasi wazawa ili kuhakikisha wanapata fursa ya miradi mikubwa hapa nchini.
Pia, amewataka kufanya kazi kwa uzalendo na ufanisi kama watanzania na kuacha ubadhilifu kwenye utekelezaji wa miradi.
Amesema kuwa uchumi wa Tanzania unaitegemea sekta ya ujenzi na uchukuzi ndio maana Rais Samia alistahili tuzo hiyo kutokana na kutekeleza nguvu katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo bababara, reli, bandari na hata viwanja vya ndege
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amewashukuru wakandarasi na wahandisi kwa kufanyia kongamano lao mkoani hapa. Mtaka amewataka makandarasi hao kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa weledi.
Tubebe matamanio ya kufanya kazi kwenye miradi mikubwa hata ya nje ya nchi. Kuna makandarasi wengi wa nje wapo nchini na sasa muone namna kutoka nje ya nchi na kutafuta kazi za ukandarasi
Mtaka.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wakandarasi Wazalendo Tanzania, Thobias Kyando amesema kuwa serikali imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya ujenzi huku wakandarasi wazawa wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Amesema kulingana na takwimu zilizopo, kati ya miradi ya Sh4.9 trilioni, wakandarasi wa ndani walipata kazi za Sh 2.9 trioni, huku wakandarasi wa nje wakipata Sh2.1 trilioni, jambo alilosema Serikali imeonesha kuwathamini wakandarasi wa ndani.
0 Comments