📌MWANDISHI WETU
WAZIRI wa elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda amewataka Wathibiti wakuu wa ubora wa shule kutoishia kujaza ripoti badala yake wafuatilie changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika maeneo yao na kutafuta ufumbuzi ili kuendelea kuboresha ukuaji wa Elimu hapa nchini.
Mkenda amewaambia maafisa hao kwamba elimu bora itapatikana na kuhakisi mahitaji ya nchi endapo kama Maafisa Uthibiti Ubora watakuwa wanaharakati wa mabadiliko katika maeneo yao ya kazi.
Pamoja na hilo,amewataka kuhakikisha malezi ya wanafunzi yanapewa kipaumbele ili kutengeneza kizazi bora kwa sasa na baadaye.
Waziri Mkenda amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha Viongozi na Maafisa wa Uthibiti ubora wa Shule makao makuu na Wathibiti Ubora wa shule Kanda na Wilaya Tanzania Bara.
Amesema Wathibiti ubora wana nafasi kubwa
katika kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na kuwataka kuendelea
kujiongeza katika utendaji kwani wao ndio mboni ya jicho la elimu
nchini.
"Nyie ni mboni ya elimu hapa nchini, mnapaswa kutunzwa, kuheshimiwa na kulindwa ili elimu iweze kuwa bora, hivyo pambaneni serikali imewanunuliwa magari 85 na mambo mengine chungu nzima yanakuja, msichoke"alifafanua.
Waziri Mkenda amewataka maafisa hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidi ili kuleta mabadiliko ya elimu nchini na kuweka alama ya utendaji kazi wao.
Kuweni wanaharakati wa mabadiliko katika maeneo yenu,..hivi unaweza kwenda kwako ukapata usingizi ikiwa shule zako hazina vitanda,wanafunzi wanalala kitanda kimoja,utapata usingizi kweli?Prof. Mkenda
Pia Prof.Mkenda amesisitiza umuhimu wa malezi kwenye shule kwani watoto wanaanza shule mapema huku wazazi wakiwa kwenye kinyang'anyiro cha maisha hivyo watoto wanakuwa katika mazingira ambayo hayaakisi ufanisi na nidhamu bora kwa mtoto.
"Tunaona kwenye mitandao mambo ya hovyo yanatokea na sisi tusingependa kupuuza tutakuja na tamko na mikakati baada ya kupitia" Amesema Prof.Mkenda na kuongeza kuwa
Waziri Mkenda amesema kuwa Uboreshaji wa elimu kwa kupitia sera ya elimu ya mwaka 2014 na mapitio ya mitaala sio ajenda ya mtu, hiyo ni agenda ya serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo maagizo hayo aliyatoa wakati akihutubia Bunge la 12 tarehe 22 Aprili 2021 Jijini Dodoma.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Prof James Mdoe amempongeza maafisa hao kushirikiti mchakato wa mabadiliko wa sera na mitaala unaonendelea nchini kwa sasa.
"Kuna zoezi muhimu sana linaendelea la kupitia mitaala na sera ya elimu na mafunzo hivyo wathibiti ubora wanapaswa kushiriki kwa kina katika zoezi hilo kw kiwango kikubwa kwani haitakuwa na maana kama msiposhiriki" amesema Prof Mdoe
Kwa upande wake Mkurugenzi wa uthibiti ubora wa Shule Mwl.Euphrasia Buchume amesema kuwa lengo kuu la kuwepo kwa idara ya uthibiti ubora wa shule ni kuhakikisha utoaji wa elimu katika ngazi ya awali,msingi,sekondari,wenye mahitaji maalum na watu wazima inafuata Sera,sheria ,kanuni ,Nyaraka na miongozo iliyopitishwa na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
0 Comments