📌RHODA SIMBA
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema deni la taifa limepanda kwa ongezeko la asilimia 14.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo Leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hali ya uchumi wa nchi pamoja na Mpango wa Maendeleo ya taifa kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Hadi Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 69.44 ikilinganishwa na shilingi trilioni 60.72 kipindi kama hicho mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.4
Aidha amesema kuwa kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 47.07 na deni la ndani lilikuwa shilingi trilioni 22.37. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na kupokelewa kwa mikopo mipya kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Amesema ongezeko la deni lilitokana na kutolewa kwa hatifungani maalumu yenye thamani ya shilingi trilioni 2.18 kwa ajili ya deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) lililotokana na michango ya watumishi wa kabla ya mwaka 1999.
Taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2021 inaonesha kuwa deni la Serikali bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa.
AKIBA YA FEDHA ZA KIGENI.
Mwigulu ameeleza kuwa akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.
Hadi kufikia Aprili 2022, akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 5.46 ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi 4.8
Waziri Huyo amesema Mahitaji ya nchi kisheria ni kuwa na kiasi cha fedha za kigeni kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa muda usiopungua miezi 4.0.
Aidha, kiwango kilichopo kinakidhi pia lengo la kuwa na miezi isiyopungua 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
PATO LA TAIFA
Amesema Ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kipindi cha mwaka, 2021 ulikuwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 mwaka 2020.
Ambapo Kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi kumetokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO–19 na uwekezaji wa kimkakati hususan katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.
Shughuli za kiuchumi zilizokuwa na ukuaji mkubwa katika kipindi cha mwaka 2021 ni pamoja na Sanaa na Burudani (asilimia 19.4), Umeme (asilimia 10.0), Uchimbaji Madini na Mawe (asilimia 9.6) na Habari na Mawasiliano (asilimia 9.1)
Pato Ghafi la Taifa lilikuwa shilingi trilioni 161.5 mwaka 2021, ikilinganishwa na shilingi trilioni 151.2 mwaka 2020. Aidha, mwaka 2021, Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu milioni 57.7, ikilinganishwa na watu milioni 55.9 mwaka 2020,"amesema.
Aidha amesema Kwa mantiki hiyo Wastani wa Pato kwa Mtu
lilikadiriwa kufikia shilingi 2,798,224.23, sawa na dola za Marekani 1,211.77
mwaka 2021 ikilinganishwa na shilingi 2,701,039.25, sawa na dola za
Marekani 1,171.51 mwaka 2020.
Amesema taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2021 inaonesha kuwa deni la Serikali bado ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu kwa kuzingatia ukomo wa viashiria vyote vinavyokubalika kimataifa.
0 Comments