WIZARA za Kisekta za Ardhi Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katiba na Sheria pamoja na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum zimekutana Jijini DSM kutafuta suluhu ya mgogoro wa Uvamizi uliofanywa katika Makazi ya Wazee Nunge yaliyoko Kigamboni Jijini DSM.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewataka wavamizi wa makazi ya wazee kuondoka mara moja na kuliacha eneo hilo kwa ajili ya malengo yaliyopangwa ambayo ni kulea Wazee.
Dkt. Chaula pia amewataka wananchi kuzingatia sheria za matumizi ya ardhi kuondokana na tabia ya kuvamia ardhi iliyotengwa kwa ajili ya matumizi maalum kama vile ardhi iliyotengwa na serikali kwa ajili ya kuwatunza na kuwatunza wazee katika maeneo mbalimbali nchini.
Nitoe rai kwa wananchi tuache kuvamia haya maeneno na nasikia watu wanajenga usiku kwa usiku sisi tutafuata Sheria Kila aliyevamia ataondoka katika hilo eneo na kuongeza kuwa vitendo vya aina hiyo mbali na kukiuka sheria vinarudisha nyuma mipango ya Serikali iliyowekwa kwa ajili ya maendeleo.
Dkt Chaula
Awali akitoa taarifa kuhusu uvamizi huo, Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii anayeshughulikia Wazee, Tullo Masanja amesema kuwa Wizara imefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha mgogoro huo unamalizika lakini wavamizi wamekuwa wakiendelea kusonga katika makazi hayo ya Wazee.
Amesema hadi sasa takribani nusu ya ardhi kwa
ajili ya makazi ya Wazee yenye ukubwa wa ekari 50 imevamiwa. Amesema hatua
mbalimbali za kuwaondoa ikiwa ni pamoja na kuwataka kuondoka kwa hiari
zimefanyika.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nhonge amesema kuwa haki itatendekea na watazingatia kwa kuhakikisha mgogoro huo unamalizika ili kila kipande cha ardhi kitumike kwa mujibu wa matakwa ya sheria za mipango iliyowekwa na Serikali.
Inapokuja kwenye maeneo ya Serikali lazima tujue kuwa maeneo haya sio ya kukimbilia na kuvamia maana unatenda kosa la jinai na hautovumilika katika hilo
Kamishna wa Ardhi.
Makazi ya Wazee Nunge, Kigamboni mkoani Dar Es Salaam ni moja katika Makazi 14 ya Wazee yanayosimamiwa na Serikali Kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa lengo la kuwahudumia na kuwalea Wazee wasio na uwezo wala ndugu wa kuwalea.
MWISHO
0 Comments