📌WMJJWM
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekubaliana
na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) kushirikiana kutafuta
namna na mbinu bora zitakazoiwezesha Tanzania kuzingatia misingi ya Usawa wa
kijinsia.
Makubaliano hayo yamefikiwa (Aprili 06, 2022) Jijini Dar Es Salaam wakati wa Kikao kati ya Wizara na Wadau wa Maendeleo kuhusu masuala ya Usawa wa Kijinsia kutoka UNFPA.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula amesema, Tanzania itahakikisha masuala yote kuhusu usawa wa kijinsia yanazingatiwa kwa kuwapa fursa wanawake katika Nyanja mbalimbali zikiwemo za uongozi na kiuchumi.
Tunaongozwa na Miongozo mbalimbali ikiwemo Dira ya Taifa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, hivyo, niwaombe tu, tuzingatie haya kwenye mipango yetu Shabaha ni twende pamoja kwa matokeo chanya na ya haraka
Dkt. Chaula
Amesema jukumu kubwa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zinazoikabili jamii ikiwemo ukatili wa kijinsia unaozidi kushamiri.
Tunasikia kila siku ukatili, mauaji sasa tushirikiane tuweke nguvu ya pamoja, tuwekeze katika elimu kwa jamii, hii itasaidia kuondokana na vitendo vya ukatili
Dkt. Chaula
Akichangia mada wakati wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amesema, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau kutafuta suluhu ya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Kwa upande wake Mshauri wa masuala ya Kijinsia kutoka UNFPA Maja Hansen amesema Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Wizara katika utekelezaji wa Mipango mbalimbali ikiwemo Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) 2017/2018-2021/2022.Mkutano kati Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na UNFPA ni muendelezo wa vikao vya majadiliano na wadau mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto za jamii.MWISHO
0 Comments