MAAFISA USTAWI WA JAMII WAPEWA MWONGOZO KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA AKILI NA SAIKOLOJIA

 

📌WMJJWM

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imesema itawekeza katika kuhakikisha huduma ya Msaada wa akili na Saikolojia inapatikana katika maeneo mbalimbali nchini ili kuisaidia jamii kuondokana na matatizo ya kisaikolojia yanayosababisha kuwepo na matatizo katika kifamilia na jamii.

Hayo yamesemwa leo Aprili 12, 2022 Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwajuma Magwiza katika kikao cha kupitia na kusambaza mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Msaada wa Akili na Kisaikolojia kwa Maafisa Ustawi wa Jamii nchini.

Bi. Mwajuma amesema kuwa mwongozo huo utatumika kuboresha Utoaji wa Huduma hiyo sambamba na kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii wanatumika ipasavyo kuisaidia jamii kuondokana na tatizo la changamoto ya akili.

Tunafahamu kwamba jamii zetu zinakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini hili la afya ya akili na matatizo ya Kisaikolojia ni mojawapo. Kazi kubwa imefanywa na Serikali ikiwepo uwepo wa Sera, Sheria na Mikakati mbalimbali ili kuondokana na tatizo hilo

Magwiza.

Ameongeza kuwa mwaka 2019 katika kipindi cha mlipuko wa Uviko 19 Wizara  ikishirikiana na Wadau mbalimbali ilitoa mafunzo kwa wataalam wa Afya katika Halmashauri 27 ili kusaidia kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa katika maeneo yao na pia  Wataalamu wapatao 423 walijengewa uwezo wa kutoa elimu hiyo kwa wajumbe wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto.

Aidha Bi. Mwajuma amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kote nchini kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo na kuzingatia yale yanayopaswa kufuatwa katika kutoa huduma za kisaikolojia kwa jamii ili kupunguza matatizo yanayoweza kutokea kutokana na matatizo ya Afya ya akili.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Baraka Makona alisema changamoto mbalimbali za kimaisha zinazoathiri akili ya binadamu zimekuwa nyingi na zinasabbisha kutokea kwa matatizo katika familia na jamii ikiwemo vitendo vya ukatili hivyo ili kuzikabili huduma za kisaikolojia zinahitajika.

Kama binadamu tumekuwa tukikabiliwa na changamoto za matatizo ya Afya ya akili, changamoto zinazotokana na magonjwa mengineyo na changamoto nyingine hivyo msaada wa kisaikolojia ni suala la muhimu ili kusaidia kutatua changamoto hizo 

Makona

Naye Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IMO) Dkt Qasim Sufi alisema binadamu wanahitaji msaada wa kisaikolojia baada ya kukumbwa na majanga mbalimbali katika maisha ya kila siku ili kuwasaidia kukaa sawa na kuendelea na maisha yao ya kila siku hivyo Shirika hilo limeunganisha nguvu na Serikali katika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana na kutolewa katika jamii ya Watanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Ustawi wa Jamii waliohudhuria kikao hicho, Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Iringa Martin Chuwa, alisema kuwa hatua ya Serikali kutoa mwongozo huo itaboresha utoaji wa huduma ya kisaikolojia kwa wanajamii kwani watoa huduma wote wa kijamii wataweza kufanya kazi ndani ya misingi na mipaka iliyowekwa na kuondokana na Wataalam kufanya tofauti kwa hisia au matakwa yao binafsi.



Post a Comment

0 Comments