📌RHODA SIMBA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi ambayo kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Akizungumza na wandishi wa habari Leo Aprili 14, 2022 jijini hapa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amesema kabla ya kilele kutatanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo maonesho, michezo na makongamano.
Nimekutana nanyi leo kuwafahamisha kuwa kwa mwaka huu Mkoa wa Dodoma umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa sherehe za Mei Mosi kitaifa ambapo zitaambatana na shughuli mbalimbali katika juma la maadhimisho kabla ya kilele ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rasi Samia
Mtaka ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa sherehe hizo amesema alikutana na wahariri wa vyombo vya habari ambao aliwafahamisha kuhusu heshima ambayo Mkoa umepata na kuwashirikisha kuhusu namna bora ya kuwa na kampeni ya hamasa lengo ni kufanya Mei Mosi ya mwaka huu ifanyike kivingine.
Amesema Mkoa umeandaa kampeni maalumu ya vyombo vya habari kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika sherehe hizo na kutumia fursa ambazo zitapatikana kupitia shughuli mbalimbali zitakazofanyika kabla ya kilele.
Ndugu zangu shughuli hii ni yetu sote kwahiyo tutumie fursa hii kutangaza Mkoa wetu ambao ni makao makuu ya nchi lakini pia shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kikao na wahariri, uzinduzi wa hashtag, michezo ikiwemo mpira wa miguu, pete, kikapu na maonyesho mbalimbali ambayo yataanza April 22 hadi 30 mwaka huu katika viwanja vya Jakaya Kikwete
Katika hatua nyingine Mtaka amesema Mkoa umeandaa nukuu mbalimbali za viongozi zilizowahi kutolewa katika maadhimisho mbalimbali ya sherehe za Mei Mosi.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA) Tumaini Nyamhokya amesema sherehe za maadhimisho ya mei mosi Kwa mwaka huu zitakuwa kivingine kwani hadi sasa maandalizi yamefikia katika hatua ya kuridhisha.
Ameshauri wataalam wanaohusika na kutoa elimu ya Sensa ya Watu na Makazi kutumia fursa hiyo kutoa elimu kupitia mikusanyiko ya watu watakaokuja kushiriki ikiwemo katika makongamano na maonyesho.
Tunashukuru sana uongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kutoa ushirikiano wa kutosha na tunawahakikishia wafanyakazi kuwa sherehe za mwaka huu zitakuwa kivingine, pia hii ni fursa kwa watu wa sensa ya watu na makazi kutumia fursa hii kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa sensa ili watu wakae tayari kuhesabiwa
Naye Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati Jane Maganga aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonyesho na makongamano yatakayofanyika kwà ajili ya kupata elimu kuhusu mikopo ambayo inatolewa na benki hiyo Kwa wafanyabiashara wadogo.
Amesema katika sherehe hizo benki ya CRDB ndio mdhamini mkuu na wataendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo utoaji mikopo ili kuboresha maisha.
Tunapenda kuwaalika wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli mbalimbali ambazo zitafanyika kabla ya kilele cha Mei Mosi na sisi kama CRDB tukiwa kama wadhamini wakuu tumejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zetu ambazo zimeboreshwa
0 Comments