📌MJJWM
WAZIRI wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dkt. Dorothy Gwajima ameyataja
mafanikio ya Wizara hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya
Sita iingie madarakani na kusema Wizara yake imepata mafanikio ya kupigiwa
mfano.
Waziri Dkt. Gwajima,
ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma Machi, 28, 2022
kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Waziri Dkt. Gwajima
alisema ndani ya mwaka mmoja Serikali ya Rais Samia, imewatambua
rasmi Wamachinga kuwa Kundi Maalum ambapo tarehe 22-23 Februari 2022, Wizara
iliandaa semina elekezi iliyofanyika Jijini Dodoma ikijumuisha viongozi 10 wa
Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) ngazi ya Taifa pamoja na viongozi 78
kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Kwenye kutekeleza ajenda ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia na malengo ya jukwaa la kimataifa la kizazi chenye Usawa, tayari Mheshimiwa Rais Samia ameshaunda Kamati ya kitaifa ya ushauri yenye Wajumbe 25 kutoka Pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar) na kufanya uzinduzi jijini Dodoma Desemba 16, 2021
Dkt. Gwajima
Dkt. Gwajima alisema
Serikali ndani ya mwaka mmoja tayari wamejenga Makao ya Taifa ya watoto yaliopo
Kikombo Dodoma yenye thamani ya Shilingi Bilioni 12.7 ambapo jumla ya watoto
250 wanahudumiwa katika makao hayo.
Waziri Dkt. Gwajima
ameyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukabiliana na vitendo vya
ukatili ambapo hadi kufikia Februari 2022, jumla ya Madawati saba (7)
yameanzishwa katika Taasisi za Elimu saba (7) ambazo ni Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Iringa,
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Chuo Kikuu
Kishiriki cha Afya cha Bugando.
Dkt. Gwajima amezidi kufafanua kuwa katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 1,843 zimeanzishwa na kufanya idadi ya kamati za hizo kufikia 18,186 kati ya Kamati 20,750 zilizokusudiwa kuanzishwa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa ifikapo Juni 2022
Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema katika kukabiliana na upungufu wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii Tasisi ya Manedeleo ya Jamii Kijitonyama, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Ufundi vimeendelea kutoa elimu kwa ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada ambapo Mwaka 2021/22, jumla ya wanafunzi 5,014 wa fani ya maendeleo ya jamii na wanafunzi 3,234 wa fani ya ustawi wa jamii walidahiliwa kwa mujibu wa vigezo vya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Jumla ya wanafunzi 4,500 walihitimu katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Vyuo sita (6) vya Maendeleo ya Jamii vya Buhare, Rungemba, Ruaha, Uyole, Mlale na Monduli pamoja na Vyuo viwili (2) vya Maendeleo ya Jamii Ufundi vya Misungwi na Mabughai. Aidha, jumla ya wanafunzi 2,493 walihitimu katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Kijitonyama
Dkt. Gwajima.
Mafanikio mengine
yaliyopatikana ni kuhamashisha jamii katika ujenzi wa nyumba bora ambapo
zimeongezeka kutoka nyumba 751 mwaka 2020 hadi kufikia nyumba 3,257 Februari
2022 ambapo nyumba hizo zilizojengwa Mikoa ya Arusha, Morogoro, Songwe,
Shinyanga, Pwani, Katavi, Mtwara, Singida na Mwanza.
Akizidi kufafanua mafanikio hayo Dkt. Gwajima alisema, Wizara imeendelea kusimamia uanzishaji na uendeshaji wa huduma za vituo vya kulelea watoto wachanga na watoto wadogo mchana, ambapo katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022, Wizara imefanikiwa kusajili vituo 303 vilivyodahili watoto 6,772 (Me 3,194 na Ke 3,578), vituo hivyo vimewezesha watoto kupatiwa huduma zinazochochea uchangamshi wa awali wa makuzi kimwili, kiakili, kihisia, kijamii na ukuaji wa lugha pamoja.
Dkt. Gwajima, alisema kutokana na maelekezo Ilani ya Uchaguzi Mkuu CCM Kifungu 93 (A na D na F); Serikali imekamilisha uundaji wa Mabaraza ya Wazee katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kisha kuunda Baraza la Taifa la Wazee na hivyo kufikia lengo la kuwa na Mabaraza 20,749. Aidha uwepo wa mabaraza hayo imesaidia kupunguza mauaji ya wazee kutoka 190 mwaka 2015 hadi 54 kufikia Februari, 2022.
Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021, wazee 758,498 (475,252 Me na 283,246 Ke) wametambuliwa ambapo wazee 508,595 sawa na asilimia 67 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF)
Dkt. Gwajima
Akiwa anahitimisha taarifa yake kwa vyombo vya Habari Dkt. Dorothy Gwajima, alitoa muelekeo wa bajeti ambapo amefafanua kuwa ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Serikali imewezesha kuongezeka kwa bajeti ya Wizara kutoka Shilingi 33,195,738,400 Bilioni, mwaka 2020/21 hadi Shilingi 43,625,929,000 Bilioni, mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la Shilingi 10,430,190,600 sawa na asilimia 31.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum ni Wizara mpya iliyogawanywa kutoka iliyokuwa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Watoto.
MWISHO
0 Comments