📌RACHEL CHIBWETE
IMEELEZWA kuwa ushiriki wa jamii na wadau mbalimbali katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia umefanikisha kupungua kwa vitendo hivyo nchini ikiwemo waathirika wa ukatili huo kupata haki zao kwenye vyombo vya sheria
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa mtandao wa kijinsia Tanzania (TGNP), Zainabu Mmari kwenye kikao cha kufanya tathmini ya mradi wa kupunguza ukatili wa kijinsia kwa asasi za kiraia 32 kutoka mikoa 13 ya Tanzania Bara na mmoja wa Zanzibar.
Mmari amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vikipingwa na kila mtu vitaisha na siyo kuiachia vita hiyo serikali peke yake.
Amesema katika kutekeleza mradi huo mtandao huo umeshirikiana kwa karibu na wadau wote wakiwemo watoto wenyewe, wanafunzi, wanawake, vyombo vya kisheria pamoja na taasisi mbalimbali za kiserikali.
Katika kipindi hiki cha robo ya pili ya mwaka tumeona mafanikio makubwa dhidi ya mapambano ya ukatili wa kijinsia ikiwemo manusura kupata huduma na watuhumiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na haki kupatikana
Ameongeza kuwa, "Mapambano ya kupinga ukatili wa kijinsia siyo ya mtu mmoja bali jamii yote inatakiwa kushiriki kwani ukatili huo husababisha ulemavu wa kudumu na hata kusababisha vifo," amesema Mmari.
Amesema mradi huo wa kupinga ukatili wa kijinsia pia unatekelezwa na serikali hivyo wadau wanashirikiana na serikali katika kutekeleza mpango huo na mafanikio yameanza kuonekana.
Naye mkurugenzi wa shirika the voice of marginalized community (TVMC), Musa Ngangala amesema ukatili wa kijinsia unazima ndoto za watoto wengi kwani ukatili huo huwasababishia madhara makubwa maishani mwao.
Amesema ukatili wa ndoa za utotoni na mimba za mapema unaua ndoto za watoto wengi wa kike kwani baada ya kubeba mimba au kuolewa kwenye umri mdogo ndoto zao hufia hapo.
Amesema ili kutimiza ndoto za watoto ni wajibu wa wazazi na walezi kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ubakaji, ulawiti kwa sababu vinadhalilisha utu wa mtoto.
Naye Hulilo Decas kutoka shirika la Kigoma Women Development Organisation (KIWODE) amesema umaskini wa kipato umekuwa ni chanzo cha waathirika wa ukatili wa kijinsia kushindwa kupata haki zao kwa sababu wanaowafanyia ukatili huo hutaka kuyamaliza ngazi ya familia.
Amesema kumaliza vitendo vya ukatili ngazi ya familia husababisha watuhumiwa kuendeleza vitendo hivyo kwa kuwa hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa zaidi ya kutakiwa alipe faini ambayo haiwezi kumaliza vitendo vya ukatili kwa mtuhumiwa.
0 Comments