UMALIZAJI KESI UKATILI KWENYE NGAZI ZA FAMILIA YATAJWA KUWA CHANGAMOTO

 


📌RACHEL CHIBWETE

WADAU wa kupinga ukatili wa kijinsia nchini wamesema changamoto kubwa inayowakumba watu wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni jamii kuwataka  kumaliza kesi hizo kwenye ngazi ya familia.

Wakizungumza kwenye kikao kazi cha kutathmini matokeo ya mradi wa kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini  wadau hao wamesema suala la jamii kutaka kesi za ukatili wa kijinsia kumalizwa ngazi ya familia linadidimiza jitihada za serikali za kutokomeza ukatili hapa nchini.

Mratibu wa mradi wa kupinga ndoa za umri mdogo na mimba za kabla ya wakati, kutoka shirika la jumuia ya kuelimisha athari za madawa ya kulevya, ukimwi na mimba katika umri mdogo (JUKAMKUM), Nassoro Ally Haji amesema mila na desturi zinadidimiza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Amesema kesi nyingi za ukatili wa kijinsia huishia ngazi ya familia ambapo waathirika wa ukatili huo hawapati haki na hata wale wanaotenda ukatili huo hawachukuliwi hatua za kisheria.

Utakuta binti amepewa mimba katika umri mdogo wazazi wa kijana aliyempa mimba wanaomba wayamalize nyumbani kwa kumuoza huyo binti, lakini baada ya muda mfupi huyo kijana anamwacha binti na kuanza kuhangaika kulea mtoto mwenyewe.
Ally Haji.

Amesema watu wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia na kesi zao kumalizwa ngazi ya familia huwa hawapati haki zao kwa sababu adhabu anayopewa mtuhumiwa huwa ndogo kuliko ambayo angepewa kwenye vyombo vya sheria.


Haji amesema kwenye Wilaya ya Chake Chake wamefanikiwa kuvunja ndoa za utotoni tisa na kuripoti kesi za ubakaji tano ambapo kesi hizo zipo kwenye hatua mbalimbali za kisheria.

Naye Mratibu wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wa SPRF kutoka Wilayani Ikungi Mkoani Singida, Paul Kigeja amesema ukatili wa kijinsia ni kosa la jinai lakini jamii huamua ziishie kwenye ngazi ya familia hali inayochelewesha wahusika wa ukatili kushindwa kupata haki yao.

Amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile ubakaji, mimba na ndoa za utotoni na vipigo vikimalizwa kwenye ngazi ya familia vitachochea watu wengine kufanya ukatili huo kwa sababu adhabu zake huwa ndogo tofauti na kwenye vyombo vya sheria.

Unamkuta mtu amempiga mke wake hadi kumsabaishia ulemavu wa kudumu lakini adhabu anayopewa ni kuchinja mbuzi nankuambiwa amuuguze mke wake mpaka apone, kwa hali hii ukatili hautakwisha
Kigeja.

Kwa upande wake Afisa habari wa shirika la mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Jackson Malangalila amesema kikao hicho kimezikutanisha asasi za kiraia 25  kutoka mikoa 14 ya Tanzania Bara na moja kutoka Zanzibar lengo likiwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto  kwenye maeneo yao.

Amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini unakomeshwa .

 

Post a Comment

0 Comments