📌MARIA ROBERT (DOMECO)
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaongoza wananchi kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati Dkt.John Magufuli.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika uwanja wa Magufuli Chato mkoani Geita ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Akizungumza kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC) baada ya ibada ya misa takatifu, Rais Samia amesema kuwa Dkt.Magufuli alisisitiza nidhamu na uadilifu katika utumishi wa umma,alipinga rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na kusisitiza uchapakazi,uzalendo wa nchi kwa ujumla.
Rais Samia amesema kuwa hayati Dkt.Magufuli alitamani kuiona Tanzania iliyo jikomboa na kujitegemea kiuchumi.
Na katika hili mtakumbuka katika hotuba yangu ya mwanzo kabisa baada ya kuapishwa nilisisitiza kwamba nitayaendeleza mema yote aliyo tuachia hayati Magufuli na kuleta mema mengine mapya kwa maslahi mapama ya Taifa letu
Aidha,Rais Samia amebainisha kwamba, baadhi ya miradi iliyoanza katika awamu ya tano imemalizika na serikali inatarajia kufungua daraja la Tanzanite lililopo Dar es Salaam ambalo ilikuwa ni ndoto ya hayati Dkt.Magufuli,amesema kuwa serikali imeendelea pia kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya,maji,elimu na umeme.
“Nataka niwaahidi Wanachato miradi hii itakapo kamilika nitakuja mwenyewe kuizindua kama alivyofanya hayati Dkt.Magufuli na niwahakikishie kuwa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda inayojengwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 34 unaendelea vizuri na baadhi ya huduma zimeanza kutolewa na ninawahakikishia kuwa tutaimaliza miradi yote na hata midogomidogo ambayo sijaitaja hapa.
Ndugu zangu tunataka kujenga Tanzania ya kisasa na kuboresha maisha ya Watanzania wote tumetoka mbali na tunakokwenda pia ni mbali na haya tubayofanya yatafanikiwa endapo tutadumisha umoja,amani na mshikamano wetu kama Watanzania.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango amesema kuwa Dkt.Magufuli alikuwa ni mwalimu wa Taifa zima na alifundisha kumtegemea Mungu katika kila jambo na kuchapa kazi na viongozi wote wakubali kujitoa sadaka kwa maendeleo ya Taifa na Wananchi.
“Tulipo kuwa na magumu ya magonjwa na mambo mbalimbali hakuchoka kulifundisha Taifa kumtegemea Mungu wakati wote na ndiyo tiba ya kweli katika shida,magumu na furaha zetu”
Naye Mjane wa hayati wa Dkt.Magufuli,Bi.Janeti Magufuli amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kuwa karibu na familia hiyo tangu wakati wa kifo cha Dkt.Magufuli na kukubali kuhudhuria katika kumbukumbu hiyo pamoja na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wote.
0 Comments