NAIBU Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
ameipongeza Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa kuanza
ujenzi wa Kampasi ya Singida ambao utaokoa kiasi cha shilingi milioni 87
zinazolipwa kwa ajili ya kupanga jengo la kuendesha shughuli zake mkoani
Singida.
Mhe. Ndejembi ametoa
maelekezo hayo mkoani Singida wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya
TPSC Singida.
Mhe. Ndejembi amesema kitendo
cha TPSC kuanza ujenzi wa Kampasi ya Singida ni maono ya kuondokana na gharama
kubwa za upangaji wa jengo wanalolitumia hivi sasa katika kutekeleza majukumu
ya chuo hicho mkoani Singida.
Ni heri mlivyoamua kujinyima ili kutenga fedha zinazotumika kujenga jengo hili, uamuzi huu ni muafaka kwani utapunguza gharama za uendeshaji wa Kampasi hii,
Mhe. Ndejembi
Aidha, Mhe. Ndejembi kwa
kutambua faida ya TPSC kumiliki majengo yake, ameielekeza Menejimenti ya chuo
hicho kuangalia uwezekano wa kujenga majengo yao katika kampasi zote ambazo
chuo kinagharamia kupanga.
Ni wakati muafaka kwa menejimenti kuona namna bora ya kuanza ujenzi katika kampasi zote mnazopanga kama mnavyofanya katika Kampasi hii ya Singida.
Mhe. Ndejembi
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Singida, Mhandisi Paskasi
Muragili ameipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora na uongozi wa TPSC kwa uamuzi wa kuanza ujenzi wa Kampasi ya TPSC Singida
ambayo itahudumia watumishi wa umma na wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kati.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi
hiyo ya Singida, Mkuu wa Chuo
na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani
Shindika amesema timu ya wataalam ilibainisha kuwa eneo hilo kutajengwa majengo
30 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Kampasi ya TPSC Singida.
Dkt. Shindika amefafanua kuwa, kutokana na gharama za ujenzi wa majengo
hayo 30 kuwa kubwa, TPSC iliamua kuwa na mpango wa ujenzi wa awamu kwa kutumia
fedha za ndani mpaka ujenzi utakapokamilika.
Jumla ya ekari 76 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida.
MWISHO
0 Comments