MHE. NDEJEMBI AWATAKA WALENGWA WA TASAF KUBORESHA MAISHA YAO ILI KUUNGA MKONO JITIHADA ZA MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

 


📌JAMES K. MWANAMYOTO

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kutumia vizuri ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao ili kuunga mkono jitihada anazozifanya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ambazo anawapatia walengwa hao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamiii (TASAF).

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo, wakati akizungumza na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Solya katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini wilayani Manyoni.

Mhe. Ndejembi amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anajitahidi kwa nguvu zake zote kupambania nchi yake anayoiongoza kwa kutafuta fedha kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wake wenye hali duni, hivyo walengwa wa TASAF wanao wajibu wa kuhakikisha wanatumia vema ruzuku wanayoipata kuboresha maisha yao ili kutokwamisha jitihada za Mheshimiwa Rais.

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anahangaika kupambania maisha yetu, sisi tunaitumia vizuri au tunaifuja fedha anayotuletea? kwani tunamuona anavyopambana kwa hali na mali hivyo ni lazima tuguswe na jitihada zake kwa kuhakikisha fedha anazotuletea kuboresha maisha yetu kupitia TASAF tunazitumia kwa lengo alilolikusudia,

Mhe. Ndejembi 

Mhe. Ndejembi hakusita kuwasisitiza walengwa wa TASAF kutomuangusha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwasababu anaendelea kupambana kila siku katika kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini.

Ameongeza kuwa, kwa namna Mhe. Rais anavyoongeza jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya walengwa wa TASAF, iwapo wakizitumia kuboresha maisha yao ana imani kuwa Serikali itaongeza muda wa kutekeleza mradi wa TASAF ili kuzikwamua kaya zote maskini nchini.

Naye, mlengwa wa TASAF katika Kijiji cha Solya wilayani Manyoni, Bi. Sarah Mangwaya ameishukuru Serikali kupitia TASAF kwa kumpatia ruzuku inayomuwezesha kumlea mjukuu wake na kumpatia mahitaji muhimu ya shule ambayo ni sare za shule, kalamu na madaftari.

Kwa upande wake, mlengwa mwingine wa TASAF katika Kijiji cha Solya wilayani Manyoni, Bw. Mkimbila Zakayo amesema, TASAF imemuwezesha kujenga nyumba mbili zenye vyumba viwili kila moja ambazo anaishi na familia yake.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya siku moja wilayani Manyoni, iliyolenga kuwahimiza walengwa wa TASAF wilayani humo kutumia vizuri ruzuku wanaoipata katika kuboresha maisha yao.


MWISHO

 

Post a Comment

0 Comments