📌MJJWM
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka Kamati za Ulinzi wa Wanawake na
Watoto zinazotekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kuweka mikakati ya kupambana na vitendo vya
ukatili vinavyotokea nchini.
Akifungua kikao na Kamati ya utekelezaji wa MTAKUWWA
mkoa wa Dodoma leo tarehe 15 Februari, 2022 Mhe. Gwajima amebainisha kuwa moja
ya changamoto inayokwamisha utekelezaji wa mpango huo ni kamati za Ulinzi wa
Wanawake na watoto katika mitaa na vijiji kutotekeleza majukumu yao.
Waziri Dkt. Gwajima amesema utatuzi wa changamoto za
ukatili unahitaji jitihada endelevu za Serikali na jamii yenyewe kwani kama
ukatili unafanywa na ndugu wa karibu, jamii inawaficha ili kuwasitiri hivyo
kamati zinatakiwa zisimame na kuzungumzia kuhusu ukatili.
Hofu ya Mungu iwepo ili watu wamrudie Mungu badala ya kuwaogopa binadamu, hatutarajii matukio kutokea na kamati zipo zisiwe na mipango ya kubaini viashiria vya ukatili
Dkt. Gwajima
Kamati za ulinzi wa wanawake na watoto 18126 zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, kata, vijiji na mitaa, mwaka 2021 ikilinganishwa na kamati 16343 mwaka 2019 sawa na ongezeko la Kamati 1843
Dkt. Gwajima
Mhe. Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Serikali ina wajibu
wa kuandaa mikakati madhubuti iliyoboreshwa itakayosaidia kuimarisha Kamati za
MTAKUWWA ikiwemo kutenga bajeti kwa kushirikiana na wadau kwa ajili ya
utekelezaji wa mpango kazi huo.
Aidha, ameiomba mikoa na Halmashauri nchini kuunda
kamati za ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto katika ngazi ya Kijiji/Mitaa mahali
ambako hazijaundwa kwa kuanza na mkoa wa Dodoma, zipewe majukumu yake kwa
usahihi na kufanya kazi kwa tija.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amezitaka Kamati kuanzia ngazi ya
Taifa kuufanya mpango kazi huu wa Taifa ujioneshe katika matokeo halisi badala
ya kubaki kwenye mafaili.
Dkt. Chaula amesema Mpango huo ulianzishwa ikiwa ni
msingi wa kutokomeza vitendo vya ukatili na kila sekta inatekeleza hivyo kwa
kuanza na Wizara inayosimamia sera na miongozo kuwe na ajenda moja na kila
mmoja asimamie eneo alilokasimiwa.
Kupitia kikao hiki nina imani tutaweka mipango thabiti kuhakikisha vitendo hivi vya ukatili na mauaji vinatokomezwa
Dkt. Chaula
Amesema baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na madawati ya
jinsia, vituo vya mkono kwa mkono na nyumba salama kwa lengo la kuwashughulikia
waathirika wa matukio ya ukatili.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Dodoma Bernard Abraham
amebainisha kuwa, chanzo kikubwa cha ukatili katika jamii ni uchumi wa kaya
kuwa mdogo, hivyo katika utekelezaji wa mpango huu, nguvu kubwa ielekezwe
kuimarisha uchumi wa kaya.
MWISHO
0 Comments