📌RHODA SIMBA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa ametoa maagizo kwa wakuu wote wa shule nchini kuhakikisha kwamba wanasimamia sheria, miongozo, na taratibu katika sekta ya elimu, kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao, pamoja na kutunza majengo ili yatumike hata katika vizazi vijavyo.
Kadhalika Bashungwa amewataka wakuu hao kuandaa motisha kwa walimu na wanafunzi ili kujenga ari ya ushindani , na kuwa viungo kati ya jamii na viongozi wanao wazunguka kwa kuishi kwa ushirikiano ambao utawasaidia katika kutekeleza kwa ufasaha miradi mbalimbali ya serikali katika jamii.
Waziri Bahungwa ametoa maagizo hayo leo February 11 jijini hapa katika hafla ya utoaji tuzo za walimu za ubora wa taaluma kwa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, kidato cha nne na kidato cha sita kwa mwaka 2021 kwa mikoa 26 ya Tanzania bara.
Amesema ili kufikia malengo ya
serikali ni lazima kusimamia miradi yote kwa ufasaha na iendane na
thamani ya fedha, na mali za shule zitunzwe kwa ufasaha ili ziweze kutumika na
vizazi vijavyo.
Wapo baadhi yenu hawana mahusiano mazuri na jamii hivyo kukwamisha utekeleaji wa baadhi ya shughuli za serikali mnapokuwa na mahusiano mazuri na viongozi katika jamii hii pia inarahisisha katika utekelezaji na hata utunzaji wa majengo ya serikaliWaziri Bashungwa.
Nae Kaimu rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Mwalimu Dina Mathamani amesema wao kama walimu wameona umuhimu wa kutoa tuzo na pongezi kwa walimu waliofanya vizuri na kuwafanikisha wanafunzi kufaulu vizuri.
“Ufaulu unaendelea kupanda siku hadi siku taaluma zinapanda na mazingira ya walimu yataendelea kuboreshwa na niahidi kwa niaba ya Chama cha walimu tutafanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka ili tupate wataalamu katika sekta mbalimbali”amesema Mwl.Mathamani.
Naye Makamu wa rais Chama cha Walimu Tanzania ambao ndiyo wadhamini wakuu wa tuzo hizo,Dinna Mathamani ametoa pongezi kwa walimu pamoja na wadau mbalimbali kwa juhudi zao zilizofanikisha kiwango cha ufaulu kinaendelea kupanda mwaka hadi mwaka.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzanaia (CWT )Mwalimu Deus Seif amesema Chama kinatambua jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha maisha ya watanzania wakiwemo walimu.
“Miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, (SGR) lakini katika Sekta ya elimu yapo mambo kadhaa ambayo serikali imeyafanya ikiwemo ongezeko la miundo mbinu na samani ,upandishwaji wa madaraja na urekebishwaji wa mishahara kwa walimu, pamoja na malimbikizo ya madeni yasiyo ya mishahara”amesema Mwl Deus.
Hata hivyo amesema pamoja na jitihada za Serikali lakini bado walimu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa nyumba za walimu, madai mbalimbali ya walimu bado yapo katika halmashauri pamoja na ajira kwa walimu.
Akizungumzia kuhusu tuzo hizo za Ubora katika Elimu,Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,TAMISEMI,Prof.Rziki Shemdoe amesema TAMISEMI ilianzisha muongozo wa utoaji wa tuzo mwaka 2019 ambapo mwaka huu tuzo zaidi ya 480 zimetolewa kwa wanafunzi,walimu na wasimamizi wa mitihani.
Kwa upande wake Katibu mtendaji Baraza la Mtihani la Taifa (NECTA) Dkt.Charles Msonde amesema jumla ya Wanafunzi 481 wamepatiwa tuzo mbalimbali baada ya kuonekana kufanya vizuri katika mitihani yao ya shule za msingi,kidato cha nne na kidato cha sita kwa mwaka 2021.
Tuzo hizo pia zimetunikiwa kwa shule 10 bora kitaifa ,walimu,mikoa,halmashauri zilizofanya vizuri na zinazoendelea kuimarika kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kadiri miaka inavyokwenda.
Dkt.Msonde amesema kwa mwaka 2021 ufaulu katika kumaliza elimu ya msingi umefikia 82.97%, mtihani wa kumaliza kidato cha nne umefikia 87.30% na kidato cha sita 99.62%.
Kauli mbiu ya Tuzo za mwaka huu inasema “Uboreshaji wa Ufundishaji na Ujifunzaji shuleni ni chachu ya kuongeza kiwango cha ufaulu wa Wanafunzi”
0 Comments