WABUNGE WAZISHAURI TAASISI ZA HABARI 'KUWAFUNDA' WAANDISHI WA HABARI

 

Mbunge wa viti maalum (CHADEMA) Ester Matiko akiteta jambo na Mwenyekiti wa MISA TAN Bi.Salome Kitomari

📌MWANDISHI WETU

BAADHI ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamezishauri taasisi za kihabari kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa Habari nchini ili kuwajengea uwezo ili waweze kufanya kazi kwa weledi.

Wakichangia katika mjadala baada ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wa sheria mbalimbali za Habari yaliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA TANZANIA),wabunge hao wameoneshwa kutoridhishwa na maendelo ya tasnia ya Habari katika siku za karibuni.


 

Wakizungumza kwa kutoa mifano ya baadhi ya Habari zinazoandikwa katika vyombo mbalimbali vya Habari nchini kuhusu suala linalofukuta la hifadhi ya Ngorongoro baadhi ya wabunge hao walisema tasnia ya Habari haijatenda haki kujulisha umma undani wa suala.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Esta Bulaya alibainisha kwamba kuna kizazi cha waandishi wa habari mahiri kinapotea lakini hakuna jitahada ya maksudi za kulea na kuibua waandishi wengine watakaofanya kazi za kusisimua na kuibua mijadala mbalimbali kwa manufaa ya nchi.

Kuna kizazi kinapotea,waandishi tulionao hivi sasa tunahitaji kuweka nguvu za ziada kwao ili wawe mahiri.,Wapo baadhi yao hawajui hata kuuliza maswali,anapokufuata anakuwekea ‘mic’ anakwambia mheshimiwa we ongea chochote tu kuhusu huu mjadala.
Ester Bulaya

Bulaya ameongeza kuwa mafunzo ya mara kwa mara yatawasaidia waandishi hao kujijenga n ahata kuongeza uwezo wao wa kuuliza maswali hivyo aliwataka MISA na Wadau wengine wa Habari kuwekeza nguvu katika hilo.

Naye mbunge wa Momba(CCM),Condester Sichwale aliwataka waandishi wa Habari kuandika Habari kwa weledi ili kuaminika katika jamii,na pia ameshauri vyombo vya Habari kujikita katika kutafuta suluhisho kwa matatizo ya yanayokabili jamii.


Tunaomba mjitahidi kusimamia maadili na miongozo inayosimamia tasnia yenu,kuna baadhi ya mambo yanakuzwa na vyombo vya habari bila sababu ya msingi na wakati mwingine Habari hizo zinaenda kupotosha jamii
Condester Sichwale

Mwenyekiti wa wabunge hao katika warsha hiyo Mbunge wa Rashidi Shangazi alisema kuna haja Tanzania kuanzishwa baraza la walaji wa Habari ili wao kama watumiaji wa Habari wawe na jukwaa la kufikisha maoni yao kuhusu muenendo wa tasnia hiyo.

“Kama walaji wengine wana mabaraza yao na sisi walaji wa Habari ni bora tukafikiria kuanzisha jukwaa letu ili inapobidi tuwaambie kwamba mnachotulisha siyo tunachohitaji.”alisisitiza Shangazi.

Shangazi pia aliishukuru MISA TAN kwa kuwajengea uwezo kundi hilo la wabunge na kuwashauri kuendelea na semina hizo kwa kamati mbalimbali za bunge ili kuwaonesha namna baadhi ya vifungu vya sheria zinazopitishwa bungeni zinavyaathiri uhuru wa tasnia ya Habari nchini.


 

Awali akifungua warsha hiyo mwenyekiti wa MISA TANZANIA Bi.Salome Kitomari alisema dhumuni kubwa la warsha hiyo ni kuwashirikisha wabunge hao mambo mbalimbali ambayo yapo katika sheria za Habari na yanachangia kudidimiza uhuru wa kujieleza.

“Tumewaita baadhi ya Wabunge wetu vinara kuwashirikisha kile ambacho waandishi wamekuwa wanakilalamikia mara kwa mara hivyo panapotokea mapitio ya sheria wawe na uzoefu na waweze kuona madhara ya baadhi ya vifungu vya sheria katika tasnia ya Habari.” Amesema Kitomari

Post a Comment

0 Comments