RAIS WA BENKI YA AfDB AHAIDI NEEMA KWA TANZANIA



📌
PETER HAULE NA SAIDINA MSANGI, WFM

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuahidi kutekeleza miradi mipya katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo na pia kuwawezesha Wanawake na Vijana kiuchumi  pamoja na ahadi aliyoitoa ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR

Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki hiyo, Dkt. Akinwumi Adesina, akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula.

Amesema kuwa Benki hiyo imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko za jijini Dodoma pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Msalato utakaojengwa mkoani Dodoma, miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amemshukuru Rais huyo wa Benki ya AfDB kwa nia ya kusaidia miradi mingine mipya kama ya Uwezeshaji wa Wanawake na vijana lakini pia uwezeshaji katika sekta kuu za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo.

Amesema maeneo hayo ni muhimu katika kukuza uchumi na yanamatokeo chanya si tu kwa watanzania lakini pia kwa Bara la Afrika kwa kuwa mradi kama wa Reli utazinufaisha nchi Jirani kwa kuwa Tanzania ina lango la Bahari hivyo miundombinu hiyo itasaidia katika kuchochea uchumi wa nchi hizo Jirani na nyingine.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameipongeza Benki hiyo kwa utendaji kazi mahili chini ya Rais Dkt. Akinwumi Adesina, kwa kuwa mwaka 2021 ilitunukiwa tuzo kwa kuwa Benki Bora Duniani katika masuala ya Fedha na pia ameshukuru kwa nia ya kusaidia utekelezaji wa miradi mipya ambayo itawasaidia watanzania.

Kwa upande wake Rais wa AfDB, Dkt. Akinwumi Adesina amesema kuwa Benki yake inatambua umahili wa Tanzania katika kusimamia sera za kifedha na kiuchumi na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kuchangia maendeleo yake katika Nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu ya nishati na barabara, kilimo, uhifadhi wa mazingira, pamoja na kuendeleza sekta binafsi.


Dkt. Adesina amesema kuwa uwekezaji wa Benki yake katika miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi hapa nchini umefikia dola za kimarekani bilioni 2.5 na kwamba Benki yake iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya hususani katika sekta ya kilimo ili nchi iweze kuzalisha chakula kwa wingi na kukiongezea thamani kupitia maeneo maalumu ya uwekezaji.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo kwa baadhi ya nchi za Afrika, Bw. Amos Cheptoo pamoja na Kaimu Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduor, ambapo kesho, Mheshimiwa Dkt. Akinumwi anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.




Mwisho.

 

Post a Comment

0 Comments