NACTVET YAVIONYA VYUO VYA KATI USAJILI WANAFUNZI WASIO NA SIFA

 

📌FRED ALFRED

BARAZA la Taifa   la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) imevionya vyuo vya kati na ufundi vitakavyosajili wanafunzi wasio na sifa katika michepuo huku vikijua kuwa vinawapotezea muda.

Hayo yamebainishwa hii leo Februari 18 jijini hapa na Mkurugenzi wa Uthibiti,Ufuatiliaji, na Tathmini kutoka NACTVET, Dk Jofrey Oleke alipokuwa  akizungumza na wamiliki wa vyuo vya afya binafsi.

Tunatoa rai kwa vyuo vizingatie mitaara wanayofundisha kuhakikisha kwamba wanaowasajili wanakuwa na sifa stahiki ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza mbeleni ikiwemo wanafunzi hao kutotambulika na baraza

Ameongeza kuwa”Tunatoa rai na tunavionya vyuo ambavyo havizingatii taratibu za udahili, na sisi kama baraza tumekuwa tukitoa adhabu kali kwasababu ukidahili wanafunzi wasio na sifa sio tu kuleta athari kwa wanafunzi bali hata kumuumiza mzazi na taifa kwa ujumla,”.

Amebainisha kuwa mwanafunzi aliyedahiliwa pasipo kuwa na sifa ni kumpotezea muda na rasilimali ambazo angezitumia kufanya shughuli nyingine ambazo alitakiwa kufanya.

Amesema pamoja na makubaliano mengine pia wameafikiana kuendeleza ushirikiano kati ya NACTVET na wadau katika masuala mbalimbali ya taaluma.

Dk Olekele amesema pia wamefikia muafaka wa kusubiri uamuzi wa Serikali katika suala la udahili wa wanafunzi kwa kipindi cha mwezi machi ambapo suala hilo lilichukua sura ya tofauti baada ya kupigwa marufuku.

Leo hii  tulikuwa   na wamiliki wa vyuo vya afya binafsi ambapo tumekutana kwaajili ya kuangalia changamoto mbalimbali katika utoaji wa mafunzo katika vyuo vyao na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Vyuo Vya Afya vya Binafsi Tanzania Dk Joel Maduhu ameipongeza NACTVET kwa kuona umuhimu wa kukutana na wadau hao muhimu ambao walikuwa na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu pasipo ufumbuzi.

Amesema wanaimaini kuwa changamoto zote zilizoibuliwa katika kikao hicho zitafikishwa mahali panapohusika na kupatiwa ufumbuzi.

“Tumefurahi kukutana na NACTVET wametusikiliza mapendekezo yetu  na tunaamini yatafika mahali panapohusika na kupatiwa ufumbuzi ili kazi zetu zikafanyike kwa weledi bila vipingamizi,”amebainisha

 

Post a Comment

0 Comments