JAPAN YAIPATIA TANZANIA BILIONI 761.8/-

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Shinichi Goto, wakisaini mikataba 

📌 PETER HAULE  NA JOSEPHINE MAJURA, WFM

SERIKALI  ya Tanzania na Japan zimesaini  mikataba mitatu ya mkopo na msaada yenye thamani ya Yen za Japan bilioni 37.9 sawa na takriban shilingi bilioni 761.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ukarabati wa Bandari ya Kigoma, uboreshaji wa miundombinu ya maji Zanzibar na Ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili.

Mikataba hiyo imesainiwa jijini Dar es Salaam, kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan, Bw. Naofumi Yamamura, kwa naiaba ya Serikali ya Japan.

Akizungumza katika hafla fupi ya kusaini mikataba hiyo, Bw. Tutuba alisema kuwa Mradi wa ukarabati wa Bandari ya Kigoma utatekelezwa kwa msaada wa Yen za Japan bilioni 2.73 sawa na takriban shilingi bilioni 54.79, ukihusisha Ukarabati wa gati za mashariki na kaskazini mwa Bandari ya Kigoma, ukarabati wa majengo ya kushushia abiria na mizigo, ukarabati wa barabara zilizopo katika Bandari hiyo na ujenzi wa majengo mapya ya abiria na mizigo.

Bandari ya Kigoma ilijengwa katika kipindi cha mwaka 1912–1927 na imekuwa bandari muhimu katika kusafirisha mizigo na abiria kwenda nchi jirani za Burundi, DR Congo, Zambia na mikoa iliyopakana na Kigoma, hivyo kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo kutachangia kuongeza ufanisi wa Bandari, kutoa  fursa za ajira, kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuchochea biashara kati ya Tanzania na nchi hizo jirani 

Bw. Tutuba

Alisema kuwa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Maji Zanzibar, utatekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Yen za Japan bilioni 10.86 sawa na takriban shilingi bilioni 218.382 ambapo mradi huo utahusisha kujenga  na kukarabati  miundombinu ya maji Mjini Zanzibar.

Uboreshaji wa Miundombinu ya Maji Zanzibar utaimarisha upatikanaji wa maji kwa kudhibiti upotevu wa maji unaotokana na uchakavu wa miundombinu ya mabomba, matangi, visima na pampu, hivyo kuwaongezea wananchi muda wa kufanya kazi, kuondoa maradhi yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama na kupunguza umasikini

Bw. Tutuba

Bw. Tutuba aliutaja mradi wa tatu uliopata mkopo wenye masharti nafuu  kutoka Japan kuwa ni  Ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili utakaotekelezwa  kwa Yen za Japan bilioni 24.31 sawa na takriban shilingi bilioni 488.667, ukihusisha pia  ujenzi wa daraja la Kikafu  lenye urefu wa mita 560, pamoja na baadhi ya barabara za Moshi Mjini.

Bw. Tutuba ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Tatu wa Miaka Mitano pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na akaahidi kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Mheshiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendeleza ushirikiano na Japan kwa faida pande zote mbili.


Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Shinichi Goto, alisema kuwa amefurahia kusainiwa kwa mikataba hiyo mitatu ukiwemo wa Barabara ya Arusha hadi Holili alioutaja kuwa ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na utachochea utangamano wa Kikanda.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan Bw. Naofumi Yamamura, alisema kuwa Japan imefungua milango zaidi ya kusadia maendeleo ya Tanzania na kuahidi kuwa Shirika hilo liko tayari kupokea mapendekezo ya miradi mingine mipya ambayo Serikali ya Tanzania itaona inafaa kupata ufadhili na mikopo nafuu.


Bw. Emmanuel Tutuba (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Shinichi Goto (kushoto) na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bw. Naofumi Yamamura, baada ya kusainiwa kwa mkataba huo.

Katika kipindi cha miaka 15 kuanzia mwaka 2006 hadi 2021, Japan imeipatia Tanzania zaidi ya yen za Japan bilioni 61.9 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.25 ambapo kati ya fedha hizo, yen za Japan zaidi ya bilioni 30.77 sawa na shilingi bilioni 620 ni misaada, na kiasi kingine cha yen za Japan bilioni 31.13 sawa na shilingi bilioni 628, ni mikopo yenye masharti nafuu.

Sekta zilizonufaika na ufadhili wa Serikali ya Japan ni pamoja na Nishati, Kilimo, Miundombinu ya barabara, Maji, na Mafunzo ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu kwa Watanzania kupitia program mbalimbali kama SDGs na ABE initiatives.

 

Post a Comment

0 Comments