FURSA YA MTAMA MWEUPE KWA WAKULIMA DODOMA

 




📌RACHEL CHIBWETE

WAKULIMA Mkoani Dodoma wametakiwa kuitumia vizuri fursa ya kilimo cha mtama mweupe aina ya mesia na tegemeo kwakuwa una soko kubwa na la uhakika ndani na nje ya nchi.

Akizungumza leo kwenye kikao kilichowakutanisha wakulima wadogo na maofisa ugani kutoka Wilaya ya Chamwino Mkoani hapa, Afisa kilimo mkuu kutoka Wizara ya kilimo, Sadoti Makwaruzi amesema mtama mweupe una soko kubwa duniani hivyo ni lazima wakulima walilime kwa wingi ili kuitumia fursa ya soko hilo.

Amesema mtama mweupe una soko kubwa kwenye shirika la chakula duniani (WFP), kampuni ya kutengeneza bia (TBL) na katika nchi za Ulaya, Afrika Kusini na Sudani Kusini.

Huu mtama mweupe uko tofauti na ule mwingine kwani una vitamini nyingi na madini mengi ambayo husaidia kuimarisha kinga za mwili na ndiyo sababu unatafutwa sana huko duniani. 

Sisi Kama serikali tumeshachunguza na kujua kuwa kuna soko kubwa la mtama mweupe na ndiyo maana tunakuja kwenu wakulima na kuwahamasisha kuitumia fursa hii kwani soko lipo kubwa ambalo hata hatujaweza kulifikia. 

Makwaruzi

Makwaruzi amesema kuwa WFP inahitaji sana mtama mweupe kwa ajili ya masoko ya nje ambapo imewekeza fedha kiasi cha Dola za Marekani million 25 ambapo kwa mwaka wa fedha 2022 pekee shirika hilo linahitaji tani 28,900 za mtama mweupe.

Amesema kwa upande wa upatikanaji wa mbegu wakulima hao wasiwe na wasiwasi kwani serikali baada ya kuiona hii fursa wameingia mkataba na makampuni 20 kwa ajili ya kuzalisha mbegu za mtama mweupe.




Kwa upande wake Afisa kutoka bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko (CPB) Mwanaidi Msangi amesema bodi hiyo pia inanunua mtama mweupe na kuongeza thamani ili kuuza nje na ndani ya nchi.

Amesema kwa mwaka 2021 bodi hiyo ilinunua tani elfu moja na kwa mwaka huu imejipanga kununua tani 3,000 za mtama mweupe kutoka kwa wakulima wa mkoa wa Dodoma.

Wakizungumza kwenye kikao hicho kilichoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Action Aid baadhi ya wakulima wameitaka Wizara ya kilimo kupeleka elimu hiyo kwa wakulima wa chini ili kuitumia fursa ya soko la mtama mweupe.

Janeth Nyamayahasi amesema elimu ya uzalishaji wa mtama mweupe kwa ajili ya soko la kimataifa inatakiwa itolewe kwa wakulima wadogo ili kusiwe na vikwazo wakati wa kuuza mazao yao

Mara nyingi huwa tunakwamishwa na ubora wa mazao tunayozalisha wakati mwingine huwa chini ya kiwango, hivyo kama serikali imeamua kutuletea hii fursa ni lazima ituelekeze na ubora wa mazao tunayopaswa kuyazalisha vinginevyo hayatakuwa na biashara bali tutaishia tuu kuyatumia kama chakula. 

Nyamayahasi

MWISHO.

Post a Comment

1 Comments

  1. Tupeni update za sasa kuhusu soko la mtama.samahani.

    ReplyDelete