ANGELA MSIMBIRA- TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na maono ya kuhakikisha anatumia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO - 19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 15,000 nchi nzima.
Akiongea katika kipindi cha Mizani kinachorushwa na TBC 1 Jijini Dodoma leo Waziri Bashungwa amesema kuwa katika Triloni 1.3 zilizopatikana kutoka mkopo huo, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitengewa shilingi bilioni 512.9 kati ya hizo fedha bilioni 304 zimejenga miundombinu ya elimu yakiwemo madarasa 12,000 kwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na madarasa 3000 kwa ajili ya watoto waliofikia umri wa kwenda shule za awali na mabweni 50 kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.
Waziri Bashungwa amewashukuru Wakuu wa Mikoa wote nchini kwa kusimamia kwa weledi ujenzi wa madarasa hayo ili yaweze kukamilika kwa wakati na kuwezesha watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuanza masomo wote Januari, 17, 2022.
Ameendelea kufafanua kuwa Serikali itaendelea kuuboresha, kuimarisha mfumo iliyopo wa kuwatumia Wakuu wa Mikoa , Wakuu wa Wilaya, Madiwani na Wakurugenzi katika kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwenye maeneo yao ili iweze kukamilika kwa wakati na kuimarisha usimamizi wa fedha zinazotolewa na Serikali kuu.
Mtegemee maboresho makubwa kwenye sekretarieti za Mikoa, tutaziimarisha ili ziweze kushuka na kusimamia Wilaya na Halmashauri katika utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo, hivyo kwa hili tumejifunza kutumia mifumo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuanzia ngazi ya vijiji na majiji yetu
Waziri Bashungwa
Amesema kuwa ataendelea kushirikiana na wakuu wa mikoa ili kuweza kuboresha mifumo ngazi ya Sekretarieti za Mikoa na kwa pamoja na Wizara ili kuweza kuzisimamia Halmashauri nchini katika utekelezaji wa Miradi ya maendeleo hasa katika suala zima la ukusanyaji wa mapato, na matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenye Halmashauri katika kutekeleza miradi mbalimbali
Amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua watumishi wabadhilifu wa Fedha za Serikali kwa kukiuka sheria na taratibu nawale wanaofanya vizuri ngazi ya Halmashauri watapatiwa tuzo za uadilifu.
Aidha, amewakumbusha Wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha watoto ambao hawajajiandikisha wanaenda shule na amewalekeza maafisa elimu Mkoa kufika kwenye Wizara zote katika Mikoa waliopo na kuwasimamia maafisa elimu Wilaya kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wafuatiliea malalamiko yaliyotolewa na wazazi kuhusu michango na kuhakikisha wanaleta taarifa Ofisi ya Rais TAMISEMI inamfikia Januari, 21, 2022
Vilevile, Waziri Bashungwa amewataka wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha vikao vilivyowekwa katika ngazi ya bodi ya shule, kamati za shule vikae na kushirikisha Wazazi na walezi katika mipango ya kuendesha elimu katika shule ili kupunguza malalamiko.
0 Comments