MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama amewataka Watendaji Wakuu wote wa Taasisi za Umma kufanya maandalizi na kusimamia utekelezaji wa mfumo mpya wa upimaji utendaji kazi kwa watumishi wa umma na taasisi zake (OPRAS).
Waziri Mhagama amesema mfumo huo ulioanzishwa mwaka 2004 kuchukua nafasi ya Mfumo wa Siri wa Utendaji Kazi uliokuwa unatumika kupima Utendaji kazi wa katika Utumishi wa Umma tangu nchi ilipopata Uhuru umeonekana kuwa na mapungufu.
Kutokana na mapungufu hayo,Waziri Mhagama ameamua kuchukua hatua za haraka za kuwaelekeza wataalamu wa Wizara hiyo kumaliza changamoto hiyo kwa kuja na mfumo mpya ambao utaanza kufanya kazi Julai 1, 2022.
Akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo jijini Dodoma kuhusu mwelekeo wa mifumo ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma,Waziri Mhagama amesema hatua hiyo imekuja ili kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa kwao wakati wa kikao chake na Mawaziri na Manaibu Waziri ambapo alieleza bayana kutoridhishwa na namna ambavyo mfumo huo wa 'OPRAS' unavyofanya kazi.
“Utendaji wa Mfumo wa OPRAS kwa sasa hauakisi hali halisi ya utendaji wa kazi wa watumishi wa Umma hali inayoleta hisia za kupendeleana au kuoneana.” Amefafanua Mhagama.
Katika kutekeleza agizo la Rais Samia tayari Ofisi yangu imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuja na mfumo wa Kielektroniki ambao utakua na manufaa kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia uandaaji wa mikataba ya kazi kwa kuwa na malengo na shabaha za kila mtumishi zitawekwa katika mfumo Rafiki na kupunguza matumizi ya karatasi.
Amesema kuwa mfumo mwingine ni mfumo wa uwazi wa kupima utendaji kazi wa taasisi ambapo unajulikana kama mfumo wa mikataba ya utendaji kazi katika ngazi ya Taasisi na ulianza rasmi mwaka 2018.
Makubaliano haya yatakuwa ni kati ya Viongozi wa Taasisi wanaosimamia katika masuala ya kisera na utendaji wa Kisera wa kila sikuWaziri Mhagama.
Ameongeza kuwa Mkataba huu unalenga kuimarisha dhana ya utendaji unaojali matokeo;kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuongeza uwajibikaji wa viongozi katika Taasisi za Umma.
Amesema mfumo huu pia umefanyiwa kazi ili uwe wa Kielektroniki ni wa makubaliano ya kimaandishi kati ya Serikali na Taasisi za Umma kuhusu malengo ambayo Taasisi husika inatekeleza katika kipindi cha mwaka mmoja.
Amesema Ofisi yake itasimamia kwa karibu utekelezaji wa mfumo huo ambao utanongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa Sera,Mikakati na Vipaumbele vya Taasisi,Sekta na Taifa kwa ujumla;kuboresha utoaji huduma kwa umma;kuimarisha utamaduni wa utendaji wa matokeo.
Pia Wizara hiyo inatarajia kuiboresha Mfumo wa Kieletroniki wa Tasmini ya Hali ya Rasilimali watu ambayo kupitia mfumo huo Serikali itaweza kukusanya taarifa za taasisi,watumishi na huduma zinazotolewa na taasisi za umma.
Kupitia Mfumo huo,Februari 2022 Serikali itaanza kukusanya taarifa na takwimu sahihi kuhusu mahitaji ya watumishi waliopo na wanaohitajika.
0 Comments