📌DENNIS GONDWE
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ameridhishwa na muitikio wa wananchi wa kata ya Makole kujitokeza kushiriki zoezi la usafi wa mazingira na kuwataka kujenga tabia ya usafi wa mazingira kwa vizazi vijavyo.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa kata ya Makole na maeneo ya jirani baada ya kuhitimisha uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira iliyozinduliwa katika ngazi ya halmashauri kwenye kata hiyo.
Niwashukuru sana, mmetoka kwa wingi sana, na bahati nzuri kabla sijaja hapa nilikuwa natembelea kwenye mitaa yenu yote ya kwenye kata. Muitikio ni mkubwa sana.Jamani usafi unaanzia nyumbani na nikisema usafi unaanzia nyumbani simaanishi nje tu, namaanisha ndani, sebuleni, chumbani kwako na maeneo ya ndani. Ile tabia ya usafi tuendelee kuijenga kwetu na kwa watoto wetu na kwa kizazi kinachokuja.
Aidha, Mkurugenzi huyo aliwapa salam za Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alieyetarajiwa kushiriki katika zoezi hilo kabla hajapata majukumu mengine ya kitaifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa kampeni hiyo imeanzia katika Kata ya Makole na zoezi la usafi linaendelea katika kata zote za halmashauri hiyo.
“Lengo la usafi huu ni kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi na nadhifu. Tunafahamu wote kuwa Dodoma ni makao makuu ya serikali, hivyo, lazima jiji liwe safi. Tunayo kaulimbiu isemayo ‘mita tano usafi wangu, usafi wangu mita tano’ ikilenga kuihamasisha jamii kufanya usafi katika maeneo yao na maeneo yanayowazunguka.” Alisema Kimaro.
Aidha, Kimaro aliwataka wananchi kutii sheria bila shuruti. “Ndugu zangu tufanye usafi katika maeneo yetu, tutii sheria bila shuruti kwa sababu sheria ndogo tuliyonayo katika Jiji la Dodoma inasema mtu asipojitokeza kwenye usafi, mtu asipofanya usafi kwenye eneo lake la makazi, taasisi na biashara, faini yake ni kati ya shilingi 50,000-200,000 au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote viwili kwa pamoja” alisema Kimaro.
0 Comments