SERIKALI YATOA SIKU 30 KWA MAKAO YA WATOTO YANAYOENDESHWA BILA LESENI

 


📌MWANDISHI WETU

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetoa muda wa siku 30  kwa Makao ya watoto yasiyo na leseni kuwasilisha maombi ya usajili katika Halmashauri husika kuboresha huduma muhimu zinazohitajika katika makao kwa kuzingatia matakwa ya kanuni

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando jijini Dodoma,Wizara imefikia hatua hiyo baada ya  Makao ya watoto 244 pekee kati ya 473 ndiyo yaliyokidhi vigezo na kupata leseni kutoka kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii huku Makao 229 yamebainika kuendeshwa  kinyume cha taratibu.

 Uendeshaji wa makao bila leseni  ni kinyume na Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009, pamoja na Kanuni zake. Hali hii inaweza kusababisha uwepo wa makao yasiyokidhi vigezo na usalama kwa Watoto

Imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009, ikisomwa na Kanuni za Uanzishaji na Uendeshaji wa Makao ya Watoto za mwaka 2012, mtu yoyote anayekusudia kuendesha makao ya watoto atatakiwa kuomba leseni ya uendeshaji wa makao hayo kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii. Ikumbukwe kwamba ni kinyume cha sheria kutumia leseni moja kuendesha makao zaidi ya moja.

Serikali inatambua jitihada kubwa za wadau wanaolea watoto walio katika mazingira hatarishi katika makao ambao wanafuata sheria, taratibu na kanuni za ulinzi na usalama wa watoto wawapo vituoni

Pia katika taarifa hiyo,Wizara imewaagiza waendeshaji wa makao ya watoto ambayo hayajasajiliwa kuhakikisha wanakidhi vigezo na kukamilisha taratibu za usajili ndani ya muda uliotolewa.

 Vilevile,Kamishna huyo ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kupitia kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kufanikisha zoezi la ukaguzi wa makao  ambayo hayajasajiliwa na yaliyokidhi vigezo na masharti ya utoaji wa huduma kwa mujibu wa sheria yaombewe usajili katika muda uliotolewa.

 Aidha, Makao ambayo yatakuwa hayajaomba usajili baada ya muda uliotolewa hatua za kisheria zitachukuliwa,pia Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali yanayomiliki makao yanaelekezwa pia kufuata utaratibu wa kupata leseni.

Maelekezo ya Vigezo na Masharti ya usajili yanapatikana katika Ofisi za Ustawi wa Jamii zilizopo Halamshauri ya Mji, Wilaya, Manispaa na Majiji pamoja na kwa Maafisa Ustawi wa Jamii waliopo Ofisi za Kata.


Post a Comment

0 Comments