📌RHODA SIMBA
WAZIRI wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt.Ashatu Kijaji amesema Serikali ipo tayari kuwawezesha wakulima wa zabibu Dodoma na kuwajengea viwanda lengo likiwa ni kuongeza mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Ameyasema hayo jijini hapa katika ziara ya kukagua maeneo ya uwekezaji ya mamlaka ya maeneo maalumu ya uzalishaji kwa mauzo ya nje (EPZA) ambapo amesema mkoa wa Dodoma ni mkoa wa kimkakati na Zabibu inayozalishwa Dodoma haiwezi kuzalishwa sehemu nyingine.
“Hatuna viwanda ikifika muda wa kuvuna Mkuu wa Mkoa unaanza kushika tumbo nawakaribisha wawekezaji waje wawekeze mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa Mikoa mitatu ya kimkakati sasa tukishazalisha zabibu zetu tunazipeleka wapi? Sisi tupo tayari kushirikiana na sekta binafsi ili tuweze kuwakwamua wakulima wetu,
Tukiachilia Zabibu tuna zao la alizeti Dodoma pia alizeti lipo kwenye zao la kimkakati tuone namna gani tunaweza kujikwamua na zao hili hata reli yetu ya kisasa inapokamilika sisi tuwapelekee mafuta
Dkt. Kijaji
Naye Mkurugenzi Mkuu wa maeneo ya uwekezaji ya mamlaka ya maeneo maalumu ya uzalishaji kwa mauzo ya nje (EPZA) Charles Itembe amesema kuwa tangu kuanzishwa kwake, Mamlaka imetoa leseni kwa Kampuni 181 ambazo zimewekeza mtaji wa jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 2.549, Mauzo nje Dola za Kimarekani bilioni 2.497 na kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 64,159 kufikia mwezi Desemba, 2021.
Aidha amesema jitihada za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kufanikisha ubainishaji na kulitenga eneo hili kwa matumizi ya kuwa Eneo Maalum la uwekezaji.
Mamlaka ya EPZ kwa mujibu wa majukumu yake Kisheria, tutaliendeleza eneo hili kama kitivo maalum cha Ugavi, Biashara na Viwanda - (Trade, logistics and industrial park) kwa kuzingatia nafasi ya kijiographia ya mkoa wa Dodoma kwa kuvutia mitaji ya uwekezaji katika sekta ya kilimo (kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa katika mikoa ya kanda ya kati kama vile alizeti, zabibu, karanga na mifugo
Charles Itembe
Aidha, sekta nyingine zinazotegemewa kuvutia uwekezaji katika eneo la mradi ni pamoja na ujenzi, madini, madawa na mavazi.
"Serikali ilianzisha Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje – “Export Processing Zones Authority” (EPZA) mwezi Februari, 2006. Uamuzi huo, ulitekelezwa kupitia marekebisho ya Sheria namba 11 ya mwaka 2002 yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kusimamia utekelezaji wa programu ya Export Processing Zone (EPZ),"amefafanua.
Sambamba na jukumu hilo, Mwaka 2008, Serikali iliiongezea EPZA jukumu la kusimamia utekelezaji wa programu ya Special Economic Zone (SEZ) kufuatia kuvunjwa kwa iliyokuwa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji. Kwa msingi huo, EPZA inasimamia utekelezaji wa programu za Export Processing Zone (EPZ) na Special Economic Zone (SEZ).
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Athon Mtaka amesema kuwa kama uwekezaji ungeanza mapema viwanda vingekuwa vingi na kuwaahidi wawekezaji kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa kila hatua kwani Tanzania inahitaji wawekezaji.
0 Comments