📌VERONICA MWAFISI
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema katika Utumishi wa Umma imezoeleka kuwa hakuna huduma bora zinazotolewa kwa wananchi jambo ambalo halijengi taswira nzuri na kuhimiza kutoa huduma bora kwa wananchi hao.
Akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga katika kikao kazi chake na watumishi hao, Mhe. Ndejembi amewataka waimarishe huduma ambazo wanazitoa kwa wananchi hao ambao ndio wateja wa Serikali wanaofuata huduma mbalimbali.
Mhe. Ndejembi, amesema kwa Serikali biashara kubwa ni utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza ni lazima wazingatie utoaji wa huduma hizo wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi.
Ameongeza kuwa, mienendo ya watumishi wa umma ni lazima ilinde taswira ya Serikali kwa kuwa wa kwanza kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Serikali na Utumishi wa Umma.
Sisi tusiwe wa kwanza kuvunja Sheria, Taratibu na Kanuni za Serikali na Utumishi wa Umma ni lazima tuzifuate
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema, hakuna wakati bora kwa mtumishi wa umma kama Kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivyo watumishi wanapaswa kulisaidia Taifa pamoja na Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Sumbawanga, Mhe. Sebastian Waryuba amemshukuru Mhe. Naibu Waziri Ndejembi kwa kuzungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuwa kila mtumishi ameguswa kwa namna yake.
Mhe. Waryuba amewaomba watumishi wa Halmashauri yake kuzingatia yale yote ambayo wameyasikia kutoka kwa Mhe. Naibu Waziri Ndejembi kwa kutoa huduma bora ili kuwa na utumishi uliotukuka.
Amesema ili wananchi wa Manispaaa ya Sumbawanga wapate faraja ni lazima kuzingatia yale waliyoelezwa ikiwa ni pamoja kuwatumikia wananchi kwa niaba ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Mkoani Rukwa, katika Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma wa Halmashauri hiyo, pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
0 Comments