📌MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria Geoffrey Pinda amewataka Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa mikoa ya Rukwa na Katavi kuwa wazalendo kwa taifa ili kuondokana na tatizo la kukatika umeme bila sababu za msingi kunakosabisha kero kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Rukwa kukagua kituo cha kupoza umeme cha TANESCO Sumbawanga ili kujua sababu za maeneo ya Mpimbwe na Majimoto kupata umeme kwa mgao wa zaidi ya masaa 12 kwa siku.
“Mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kavuu nimeambatana pamoja na wananchi toka Majimoto na Mpimbwe kuja hapa Sumbawanga ambapo ndio umeme wetu pia unatoka kuangalia tatizo gani linapelekea kuwa na mgao wa zaidi ya masaa 12 hatua inayofifisha uchumi wa wilaya yetu pia Taifa “alisema Naibu Waziri Pinda.
Naibu Waziri Pinda alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa Rukwa na Katavi na taasisi zake ili kutatua changamoto za umeme katika Jimbo la Kavuu Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
Eneo la Majimoto kule Mpimbwe kuna jumla ya viwanda 55 vya kuongeza thamani zao la mpunga ambavyo vimesimama kufanya kazi kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika toka Tanesco hatua inayopelekea hasara kwa wafanyabiashara pia serikali uchumi unadidimia.
Pinda.
“Toka Majimoto tunapeleka mchele nchi za Uarabuni, India, Pakistan , hivyo kitendo cha kutopatikana umeme kunaleta hasara kubwa kwa watu wetu .Rais Samia Suluhu Hassan katoa maelekezo umeme upatikane ili uchumi ukue, Tanesco mna jukumu hilo kwa Taifa” alisisitiza Naibu Waziri Pinda.
Kufuatia hatua hiyo Naibu Waziri Pinda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kavuu mkoa wa Katavi alitoa wito kwa Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Rukwa Mhandisi Japhet Malongo kufanya uchunguzi wa malalamiko kuwa baadhi ya watumishi wa TANESCO Wilaya ya Nkasi kudaiwa kusababisha mgao wa umeme kinyume cha utaratibu uliowekwa na shirika.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akizungumza kwenye kikao cha Naibu Waziri huyo na watendaji wa TANESCO alisema changamoto za upatikanaji umeme Rukwa zinatakiwa kuwa wazi kwa wananchi kujua ratiba za mgao huo.
Mkirikiti alibainisha kuwa umeme unaopatikana Rukwa na kusambazwa hadi wilaya za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo na Mpimbwe mkoa wa Katavi unatoka nchini Zambia ambapo kituo cha kupokea kipo Sumbawanga ambapo kwa sasa kumekuwa na tatizo la mgao.
Nia ya serikali ni njema katika kutatua changamoto hii mgao wa umeme kwa sasa Tanesco inakamilisha mradi wa ujenzi wa transfoma kubwa itakayozalisha umeme wa megawati 15 zitakazoongeza uwezo wa kuhudumia mikoa ya Rukwa na Katavi ifikapo mwisho wa mwezi Februari mwaka huu
RC Mkirikiti.
Naye Meneja wa Mradi wa kuboresha kituo cha umeme Sumbawanga Mhandisi Albert Msangi alisema mradi huo unahusisha kujenga transfoma kubwa mpya na kujenga njia za umeme nne kwa wateja ambapo utawezesha kuongeza megawati 15 za umeme toka 10 za sasa.
Mhandisi Msangi aliongeza kuwa mradi huo unagharimu serikali shilingi Bilioni 3.8 na utakamilika mwezi Februari mwaka huu ambapo Tanesco imelenga kuondoa changamoto ya upatikanaji umeme Sumbawanga na Halmashauri ya wilaya zake ikiwemo Mpimbe Katavi.
“Tanesco ina mradi mwingine mkubwa wa kuunganisha Sumbawanga na gridi ya taifa unaonzia Iringa kupitia Mbeya hadi Tunduma kisha kuja Sumbawanga ambapo utakuwa na msongo wa kilovoti 400 chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia na kazi ya kutafuta mkandarasi imeanza” alisema Mhandisi Msangi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Majimoto Jonas Andrew alisema ili kujitenga na madai ya siyo na tija kuhusu vita ya kibiashara kati ya wafanyabiashara wa Sumbawanga na Mpimbwe ,Tanesco waweke wazi taarifa na ratiba za mgao wa umeme.
Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe iliyopo wilaya ya Mlele inapata umeme kutoka kituo cha kupoza umeme kilichopo Sumbawanga mkoa wa Rukwa.
Imeandaliwa na;
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa,
SUMBAWANGA
0 Comments