📌PRISCA ULOMI, WHMTH.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa hakuna uongozi wa mtu mmoja, menejimenti ya mtu mmoja, tushikamane kwa pamoja kwa mafanikio ya Wizara ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika kutumikia wananchi
Dkt. Yonazi ameyasema hayo kwa wajumbe wa menejimenti ya Wizara hiyo wakati wa makabidhiano ya Ofisi baina yake na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum
Amewaeleza wajumbe hao kuwa, nafasi tulizonazo ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu hivyo amewaasa kila mmoja kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuwa wapo watanzania wengi wenye uwezo zaidi yao na wahakikishe utendaji kazi na lolote litakalofanyika kupitia mikono ya watumishi wa Wizara lifanyike kwa nguvu zote, bidi na akili zote katika kutekeleza majukumu ya Wizara
Amemhakikishia Dkt. Chaula kuwa Wizara ipo mikono salama kwa kuwa wamefanya kazi kwa pamoja, amewafundisha kujali watumishi na wananchi au mtu anayedai Serikali alipwe haki yake na watumishi waishi kama familia kwa kushikamana katika kutumikia wananchi
Naye Dkt. Chaula ametoa rai kwa menejimenti ya Wizara hiyo kuwa waendelee kufanya kazi kwa matokeo makubwa ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao utajengwa kwa urefu wa kilomita 4,442 na utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi kwenye maeneo mbalimbali nchi nzima kwa kuwa Serikali, sekta binafsi na wananchi wanategemea TEHAMA katika kuendesha shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutawala
“Utendaji kazi mzuri wa Dkt. Yonazi unawategemea ninyi, nashauri mtembee pamoja, mshirikiane na kutekeleza Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2021 2026; Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025; kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za Serikali ili kufanikisha azma ya Serikali ya kutumikia wananchi kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari”, amesisitiza Dkt. Chaula.
Kikao hicho cha makabidhiano hayo kimefanyika leo kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo uliopo Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma na kushuhudiwa na wajumbe wa menejimenti wa Wizara hiyo kufuatia mabadiliko aliyoyafanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuteua Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu; na Manaibu Katibu Wakuu mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
0 Comments