WHITIMU UTUMISHI WAKUMBUSHWA UMUHIMU WAO KATIKA UJENZI WA TAIFA

 


📌JAMES MWANAMYOTO

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutambua kuwa wana umuhimu mkubwa katika ujenzi wa taifa, kwani taifa haliwezi kujengwa na wasomi wenye shahada za uzamili na uzamivu pekee, hivyo kila mhitimu kwa taaluma aliyonayo anayo nafasi ya kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo mjini Singida wakati wa Mahafali ya 34 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) yaliyofanyika mkoani humo.

Mhe. Mchengerwa amesema, taifa letu linapaswa kujengwa na kila Mtanzania, awe ni Dereva, Katibu Mahsusi, Mhudumu au Karani na ndio maana watumishi wa kada hizi za chini ndio walitumiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa harakati za ukombozi kwani wana mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inawathamini na itaendelea kuwathamini wahitimu hao ikiwa ni pamoja na kumthamini kila Mtanzania anayehitimu kwani elimu wanayoipata ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa.



Mhe. Mchengerwa amesema kazi zinafanyika kwa kutegemeana na kuongeza kuwa Kiongozi wa ngazi ya juu hawezi kutekeleza wajibu wake ipasavyo kama hana Katibu Mahsusi, Mhudumu au Dereva anayemsaidia kutekeleza majukumu yake kikamilifu, hivyo kila mmoja wetu anamtegemea mwenzie kutimiza majukumu yake kwa mustakhabali wa taifa.

Kwa kutambua kuwa kila mmoja ana mchango katika ujenzi wa taifa imara, Mhe. Mhengerwa amewaasa wahitimu hao kujiendeleza kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania pindi watakapokuwa na uhitaji huo.

Msisite kujiendeleza, wenye cheti wapate stashahada, na wenye stashahada wapate shahada na mkihitimu mkaudhihirishie umma kuwa ninyi ni watu muhimu katika ujenzi wa Tanzania ambayo Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekusudia kuijenga

Wzairi Mchengerwa

Awali, akitoa neno la utangulizi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka amesema chuo kitaendelea kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Serikali inapata watumishi wenye weledi na uwezo wa kutoa mchango utakaoleta maendeleo katika taifa.

Akiwazungumzia wahitimu, Dkt. Turuka amesema anatumaini kuwa wahitimu hao wamepikwa ipasavyo na wako tayari kulitumikia taifa kwa kutumia ujuzi kwa uadilifu na weledi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Post a Comment

0 Comments