📌RHODA SIMBA
WADAU wa mradi wa
mapambano dhidi ya rushwa ujulikanao “Tuungane kutetea Haki awamu
ya pili unaotekelezwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa
nchini[TAKUKURU] kwa kushirikiana na shirika la Konrad Adenauer
Stiftung[KAS] kutoka nchini Ujerumani wameitaka taasisi hiyo kuongeza kasi ya
kusambaza elimu ya rushwa katika ngazi za chini katika jamii.
Wadau hao ni pamoja na
Viongozi wa TAKUKURU Mkoa,na Wilaya viongozi wa dini sambamba na
waratibu vitengo vya taaluma za rushwa wamesema vitendo vya rushwa vinaweza
kukoma ikiwa kila mwanajamii ataelewa madhara na kuchukia rushwa.
Kadhi wa Mkoa wa
Dodoma Kisusu Mvumbo ameshauri TAKUKURU
katika kuendeelea na mapambano hayo dhidi ya rushwa watoa elimu watembelee
nyumba za ibada na kuomba kutumia japo dakika 15 kuelimisha waumini kuhusu
rushwa.
Mvumbo amesema pamoja
na kutoa elimu hiyo kanisani na misikitini lakini pia watumie vyombo vya habari
zikiwemo radio na televisheni kuielimisha jamii kujua haki zao ili kusiwepo na
mianya ya utoaji wa rushwa.
Mwenyekiti kamati ya
Maadili ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Ombeni Msuya amesema TAKUKURU
kupitia watoa elimu waendelee kusambaza elimu ya rushwa katika vyuo kwa
wanafunzi ili waelewe haki zao na kujua namna ya kutopokea au kutoa rushwa.
Tunaona kiukweli jitihada ambazo TAKUKURU wanazifanya lakini elimu hii isambazwe kwenye vyuo ili wanafunzi wetu waendelee kuelewa rushwa ni nini
Dk.Msuya.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa kikao hicho Dkt.Francis Michael ambaye ni Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amekiri umuhimu wa mapendekezo ya sheria ya
rushwa ili kutoa adhabu zaidi kwa viongozi wala rushwa.
Sheria hiyo kwa sasa
inaelekeza kutaifishwa kwa mali za viongozi ambao watakutwa na hatia ya kupata
mali hizo kwa vitendo vya rushwa.
Utaratibu huu wa kuwataifisha mali zao halafu wanaendelea na shughuli zao kiukweli haijakaa sawa na haitoi hofu kwani mtu anajua nikitaifishwa mali zangu ajira yangu inabaki kuwa pale pale TAKUKURU inabidi ikae itazame upya sheria hii
Naye Naibu Mkurugenzi
Mkuu wa TAKUKURU nchini Neema Mwakalyelye amesema lengo la mradi wa
tuungane ni kuwashirikisha wadau ngazi za vijiji na mitaa hadi Taifa namna ya
mapambano dhidi ya rushwa huku meneja mradi wa KAS Tanzania Damas Nderumaki
akisema matarajio ya sasa ni kufikia mikoa 24 .
“Tumejipanga kusambaza
elimu hii mashuleni,misikitini,makanisani, watendaji wa mitaa kuwashirikisha
katika vikao vya halmashauri na pia mtaala mashuleni tunaendelea
kujipanga elimu hii ianzie katika shule ya msingi ili watoto wawe na
uelewa kuhusu rushwa”amesema Neema
Kwa upande wao baadhi
ya wadau wa mradi wa Tuungane akiwemo Naibu Kamishina Mkuu wa Skauti Tanzania
Abdallah Sakasa,mbunge wa Mbagala,Abdallah Chaurembo pamoja Afisa
Uchunguzi TAKUKURU Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Ilandike Julius
wamesema kikao hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya
rushwa .
Wamefafanua kwamba kupitia
mapendekezo yaliyotolewa katika kikao kazi hicho yakiwemo ya kutoa elimu
katika jamii ikiwemo misikitini,makanisani, shuleni na mitaala kuangaliwa upya
wanaamini ya kwamba endapo yatatekelezwa kwa ufanisi kwa kiasi kikubwa watakuwa
wamejitahidi katika mapambano dhidi ya rushwa .
0 Comments