UZALISHAJI SAMAKI WA ZIWA TANGANYIKA WAJA KIVINGINE

Na Jasmine Shamwepu.

Uvuvi unaoendelea kwa miaka mingi katika Ziwa Tanganyika ulihusishwa na mila na desturi zilizopitwa na wakati ikiwemo ushirikishwaji mdogo wa wanawake, uvuvi haribifu ulishamiri na kusababisha  uharibifu wa mazingira na kuhatarisha afya za walaji wa samaki huku wakipoteza mazao mengi kwa kukosa hifadhi na usimamizi bora.

Mazao ya uvuvi hasa dagaa walianikwa chini kwenye mchanga  na kusababisha kukosa ubora. Baadhi ya wavuvi waliendesha uvuvi kwa kutumia zana duni, haramu na zisizo na tija na hivyo kupoteza muda mwingi bila kunufaika na sekta hiyo.

Agnes Salleh, mkazi waTarafa ya Karima, Mkoani Katavi ambaye pia ni mchakataji wa mazao ya samaki anataja changamoto kwenye gharama za majiko huku mwenyewe akitumia jiko lenye moshi na kulazimika kukodi chanja kwa gharama kubwa ili kukausha mazao yake.



“Kuanika chini kunatukosesha wateja kutokana na viwango duni vya uzalishaji wa dagaa,” anafafanua na kuongeza kuwa umefika wakati kwa Serikali kuwawezesha kwa mafunzo na mikopo yenye masharti nafuu kupitia kwenye vikundi.

Cosmas Matala ni mvuvi kutoka Kasanga, Kalambo Mkoani Rukwa anakiri kuwa uvuvi duni umesababisha maendeleo duni wa sekta hiyo huku akitaja changamoto kubwa ya ukosefu wa masoko ya kuuza samaki, “Ubora wa samaki unapotea kwa kuharibika kutokana na muda mrefu unaotumika kuwapata samaki na kuwafikisha kwenye soko.”

Pamoja na changamoto hiyo, bado wavuvi wanatumia mitumbwi ya kusukuma kwa makasia ambayo hayawezi kufika kwenye maeneo muhimu kwa wakati.

Mdau mwingine Vangelina Yeremiah anasema pamoja na bei kupanda kila wakati bado anatumia beseni kichwani kutembeza samaki kwa vile hakuna masoko huku akipendekeza Serikali iwekeze katika ujenzi wa masoko.

Vangelina ambaye pia ni mchakataji wa samaki kwa kipindi cha miaka 15, anasema anapata mafanikio madogo kutokana na mtaji usiotosheleza mahitaji ya biashara na gharama za uendeshaji wa familia, “Serikali ituangalie katika upatikanaji wa mitaji kwa kuwa tunashindwa kumudu mahitaji ya familia kwa kutumia mitaji yetu midogo ambayo inakatika,” anaweka wazi maombi yake.

Wizara ya mifugo na uvuvi nchini imeweka mkakati wa kukabili changamoto mbalimbali za wadau wa sekta ya uvuvi ili kuongeza  mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.



Akifungua warsha ya siku mbili ya kujadili rasimu ya mpango mkakati wa kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi (dagaa, migebuka na lumbu) wa Ziwa Viktoria chini ya mradi wa FISH4ACP – kwenye ukumbi la Social Hall Desemba 6-7, 2021 mjini Kigoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Dkt Rshid Tamatamah ametaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara za mazao ya uvuvi na kudhibiti uvuvi haramu.

Amesema Serikali pia imezuia utoroshwaji holela wa raslimali za uvuvi, kuwezesha uvuvi endelevu na kuboresha kanuni za uvuvi kwa kufanya mapitio ya tozo na kupunguza gharama za uendeshaji kwa wadau wa sekta hiyo ili waweze kumudu na kuhimili ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi.

“Kwa mfano, mwaka 2020 Serikali ilipunguza viwango vya tozo ya usafirishaji wa dagaa na migebuka kwenda nje ya nchi kutoka Dola 1.5 hadi Dola 0.5 kwa kilo ya dagaa na Dola 0.5 hadi Dola 0.3 kwa kilo ya samaki aina ya migebuka” anasema Katibu Mkuu.

Katika hatua nyingine Serikali imeweka msisitizo mkubwa kuhakikisha raslimali za uvuvi zinavunwa kwa uendelevu na usimamizi makini na shirikishi wa raslimalikwa kutegemea uwepo wa taarifa sahihi za wingi wa samaki na mtawanyiko wake katika maji nchini kote bila kujali ni bahari, ziwa, mito au mabwawa ya samaki.

Katika utekelezaji wa dhana ya uvuvi na usimamizi endelevu, Serikali ya Awamu ya Sita imetenga fedha kwa ajili ya utafiti ili kutambua wingi na mtawanyiko wa samaki katika Bahari ya Hindi na Ziwa Tanganyika katika mwaka huu wa fedha  2021/2022.



Warsha ya wadau ya kuthibitisha Dira na Mpango Mkakati wa Kuendeleza mnyororo wa Thamani wa Dagaa, Migebuka na Lumbu wa Ziwa Tanganyika hiyo ilihudhuriwa na wawakilishi wa taasisi na mashirika ya kimataifa  wakiwemo wawakilishi wa FAO kutoka Ethiopia, Martin Van Der Knaap, Afisa Uvuvi na viumbe maji wa Shirika hilo Kanda ya Afrika, na Giang Duong, bingwa wa masuala ya mnyororo wa thamani, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Bwana Andrea Massarelli,  Dkt Emmanuel Magese Bulayi, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka makao makuu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dkt Ismael Kimerei na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kogoma, Injinia Dkt Rashid Mchatta. Wengine ni wadau kutoka mikoa ya Rukwa, Katavi na wenyeji kutoka Kigoma wakiwemo wavuvi, wachakataji wa samaki na wasafirishaji.

Kwa mujibu wa Dkt Tamatamah, utafiti upande wa ukanda wa uchumi wa bahari  (EEZ) unafanyika kwa mara ya kwanza nchini tangu kuwekwa kwa misingi ya Taifa na kwamba utafiti huu utawezesha kufahamu kwa kina kiasi cha samakiwaliopo majini na kiasi cha samaki watakaovunwa bila kuathiri uendelevu wa raslimali hizo.

Hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 800 zikiwemo shilingi milioni 137 zitakazotumika kufanya utafiti wa wingi na mtawanyiko wa samaki katika Ziwa Tanganyika, “Ni fedha kidogo za kufanyia kazi ya utafiti kwa msimu mmoja” anasema Katibu Mkuu na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali ili kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi katika vipindi viwili vya kiangazi na masika.

Kuhusu changamoto za Sekta hiyo ya uvuvi, Serikali imeainisha maeneo kadhaa yanayohitaji uwekezaji mkubwa kwa lengo la kukabiliana na vikwazo, matatizo na changamoto za uendelezaji shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika.



Anataja ukosefu na uchakavu wa miundombinu ya uvuvi hasa mialo ya kupokelea samaki na masoko, kutopatikana kwa  mikopo ya kutosha na yenye masharti nafuukwa wavuvi na wachakataji ikilinganishwa na mahitaji makubwa yaliyopo na  vilevile kuendelea kuwepo kwa upotevu wa mazao ya uvuvi baada ya uvunaji wake ambao unakadiriwa kufikia asilimia 40 hususan nyakati za masika.

Changamoto nyingine ni pamoja na majanga ya asili yakiwemo mafuriko na mabadiliko ya tabia nchi ambapo mfano wake ni katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ambako mialo kadhaa (ukiwemo wa Kibirizi) imezama kwenye maji na kusababisha kushindikana kutumika kama ilivyokusudiwa na hata madarasa yawanafunzi wa chuo cha mafunzo ya uvuvi na ughani yalihamishwa baada ya kuathirika kwa hali eneo hilo.

Katika hatua za kukabiliana na majanga na changamoto hizo Serikali kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo katika Sekta hiyo wameanzisha Mradi mkubwa wa FISH4ACP ambao unatarajiwa kuja kutatua changamoto hizo  katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mzima wa miaka mitano kuanzia mwaka 2020-2024.

Dhima kuu ya mradi huo ni kujibu hoja moja kwa moja kuhusu changamoto za wadau wa sekta hiyo katika ngazi zote kwa kuzingatia mnyororo wa thamani kutoka kwa mvuvi hadi kwa mlaji wa samaki.



Wizara ya mifugo na uvuvi imeainisha lengo kuu la mradi huo kwa kuzingatia mpango wa tatu wa maendeleo wa miaka mitano (FYDR-III) ambao ulizinduliwa mapema mwaka huu (2021).

Mradi huo unagharimiwa kwa hisani ya Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na Shirikisho la Wizara ya Uchumi na Maendeleo la Ujerumani (BMZ) na utekelezaji wake unafanyika katika nchi 12 za Jumuiya ya Nchi za Kiafrika, Karibiani na Pasifiki (OACP) wenye lengo la kuchangia upatikanaji wa chakula na protini ya uhakika.

Nchi hizo pia zinalenga kuongeza nguvu ya uchumi na kutengeneza ajira ili kujenga uchumi wenye mazingira endelevu na ushirikishwaji wa jamii kwenye sekta ya uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji kwa nchi wanachama.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo 12 ambayo mnyororo wa thamani wa dagaa na migebuka kutoka Ziwa Tanganyika ulibahatika kuingizwa kwenye programu ya utekelezaji wa mradi baada ya kushindana na nchi nyingine zaidi ya 40.

Katika kipindi cha awamu ya kwanza (2020/2021) mradi ulijikita  zaidi katika kukusanya taarifa na maoni kutoka kwa wadau na kuzifanyia uchambuzi wa kina ambao umesaidia kupata rasimu ya mpango wa maboresha ya mnyororo wa thamani.

Aidha, baadhi ya mambo makubwa yaliyofanyika katika mchakato wa awali ni kuandaa na kuthibitisha matokeo ya awali ambapo makubaliano maalum yalifanyika huku lengo kuu likiwa ni kuthibitisha matokeo ya utafiti uliokuwa umefanywa na TAFIRI na FAO na kuweka vipaumbele vya kazi zitakazotekelezwa katika kuboresha na kuendeleza mnyororo wa thamani.

Tayari warsha kadha zimefanyika ikiwemo ya Agosti, 2021 ambapo pamoja na mambo mengine iliainisha maeneo ya kimkakati kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza mnyororo wa thamani wa dagaa na migebuka wa Ziwa Tanganyika.

“Tulibainisha shughuli mahususi za uwekezaji na majukumu ya kila mdau kwenye mradi,” sehemu ya rasimu hiyo imefafanua huku Katibu Mkuu akihimiza wadau kuzingatia sheria na mipango waliyojiwekea, “Mkiandaa mpango bora unaotekelezeka, utakuwa na tija ya kuwainua wadau wa uvuvi kiuchumi, kuongeza ajira na kupunguza umaskini na hatimaye kuweza kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) na malengo mengine ya kikanda, kibara na kimataifa” anafafanua Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt Tamatamah.



Anatoa shukrani kwa Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani (BMZ) kwa kukubali kugharimia mradi huo kupitia Jumuiya ya Nchi za Kiafrika, Karibiani na Pasifiki (OACP) na wakati huo huo kupongeza Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) kwa kusimamia utekelezaji wa mradi wa FISH4ACP kwa niaba ya Wizara yake na Serikali kwa ujumla.

Naye Emanuel Magese Bulaya, Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya ufugaji  na uvuvi anasema mradi huo utanufaisha wavuvi, wafanyabiashara wa samaki na wanawake, kati ya wadau wengine na kwamba Serikali inakusudia kuweka msisitizo katika utaalam, utafiti na sheria.

“Lengo kuu ni kuhakikisha mradi unatekelezeka kwenye ngazi zote zenye usimamizi na wataalam katika ngazi ya halmashauri, mkoa na Taifa na hivyo kusaidia wvuvi na wafanyabiashara wasije kupata hasara kwa kukosa taarifa na elimu juu ya raslimali na uvuvi endelevu kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi. Tunataka taarifa ziwafikie wadau wote,” anasisitiza Magese Bulaya.

Mratibu wa Mradi wa FISH4ACP kutoka FAO-Tanzania Bw Hashim Muumini anazungumzia mpango wa kufungua fursa za uvuvi katika Ziwa Tanganyika kwa kutumia Mradi wa FISH4ACP  katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa kuzingatia misingi iliyowekwa kutokana na stadi zilizoangalia kwa kina changamoto zinazokabili mnyororo wa thamani kutoka kwa mvuvi hadi kwa mlaji.

Anasema mradi huo unaohusisha wadau kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma unahusisha samaki aina ya dagaa, lumbu na migebuka wa Ziwa Tanganyika na utekelezaji wake unategemea mapendekezo ya wadau ya kukabili changamoto zao.



Muumin anatoa wito kwa wadau kuupokea mradi wa FISH4ACP kwa vile unatokana na mapendekezo na maoni yao ambayo yamechambuliwa kwa kina ili kufanyiwa kazi. “Huu ni mradi kwa ajili yao na kwamba unatekelezwa kuanzia ngazi ya mvuvi hadi kwa mlaji wa samaki. Kiujumla miradi inayotekelezwa na Umoja wa Mataifa hushirikisha watu wote, wakiwemo wanawake, watu wenye ulemavu na vijana.”

Kwa mujibu wa Muumin athari za utamaduni katika maeneo mengi yenye miradi ya maendeleo bado inawaacha watu wa makundi maalum bila kuwashirikisha na mradi huu umebainisha kuwa ushirikishwaji wa wanawake na wasichana ni mdogo.

Katika utekelezaji wa mradi, mikakati imeandaliwa kutoa elimu kwa wanawake na vijana ili kuongeza ushirikishwaji wao na ushiriki wao katika usimamizi na utekelezaji kwa kuwashirikisha katika maamuzi ya uwekezaji. “Kimsingi mradi umeandaa afua maalum inayohusiana na masuala ya usawa wa kijinsia kwa ajili ya wanawake na wasichana.  

Mapema Mtaalam kutoka FAO, Giang Duong ambaye ni bingwa katika masuala yamnyororo wa thamani anasema katika utekelezaji wa majukumu ya mnyororo wa thamani mradi hauna budi kuzingatia masuala ya jinsia hasa baada ya kubainika kwenye stadi za awali kuwepo kwa changamoto ya ushiriki mdogo wa wanawake na wasichana.

“Itafanyika stadi nyingine ambayo itaendeshwa chini ya mradi huu, ili kubainisha suluhisho la changamoto zinazowakabili wanawake,” anasema Giang Duong na kuongeza kuwa mapendekezo yatakayotokana na stadi hiyo yataingizwa kwenyempango wa utekelezaji wa mradi katika hatua zote kwa kuhusisha suala la jinsia katika afua zote.



Hatua hiyo itasaidia wanawake kujengewa uwezo na kupewa mafunzo katika vikundi vya uzalishaji na uchakataji mazao ya uvuvi, kupewa fursa ya kupatamikopo yenye masharti nafuu na kuangalia kwa undani sababu za ushiriki mdogo wa wanawake na wasichana katika usimamizi wa raslimali mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uvuvi, ardhi na mnyororo wa thamani.

Francis John ni Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Wavuvi Tanzania na mdau wa uvuvi katika Ziwa Tanganyika, anapokea mradi huo kwa mikono miwili huku akiamini kuwa utaleta mabadiliko makubwa.

“Watu watabadilika na biashara ya mazao ya uvuvi sasa itashamiri na kuleta mageuzi makubwa kiuchumi na kwa lishe ya watu wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.”

Anasema baada ya mafunzo ya mnyororo wa thamani hakuna mvuvi wala mfanyabiashara atakayeanika samaki chini, na kwamba miundombinu muhimu ikiwemo ujenzi wa maabara utasaidia kupima ubora wa mazao kabla ya kusafirisha kwenye soko la ndani na nje ya nchi. “Watu watakula chakula chenye ubora na hayo ni matunda ya mradi.”

Anasema mabadiliko mengi yamekwishaanza kuonekana huku Benki ya Kilimoimeanza kutoa kwa wavuvi huku ikiwa tayari imeshakabidhi barua kwa vyama vilivyokidhi vigezo na kuwa tayari kupata mikopo yenye masharti nafuu.

Post a Comment

0 Comments