📌RHODA SIMBA
NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia afya Dk.Grace Magembe amewaagiza maafisa afya wote nchini kwenda kusimamia sheria, kuhakikisha kwamba kila kaya nchini inakuwa na choo bora.
Aidha amesema asilimia 70 iliyopo ya kaya zenye vyoo nchini ni ndogo maafisa hao wakasimamie kuhakikisha inafikia asilimia 100 kwani suala la nyumba kuwa na choo ni lazima siyo hiari.
Ameyasema hayo leo Disemba 15 jijini hapa wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa afya, Mazingira na usafi,Mkutano ambao umeratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) pamoja na wadau wa maendeleo nchini.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa taaluma ya maafisa afya nchini kwani suala la kulinda afya katika jamii inafanywa na maafisa afya hasa katika magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa uviko 19,ebola kipindu pindu na maradhi mengine.
“Nachukua nafasi hii kuwapongeza maafisa afya wote nchini, huwa nasema ninyi ni maafisa usalama kwani shughuli mliyoifanya kwenye kipindi cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona mmeifanya kazi kubwa mmesimamia jamii wameelewa namna ya kujikinga na kufata maelekezo ya namna ya kujilinda na ugonjwa wa Covid mpaka nchi yetu kutoingia kwenye marufuku ya kutotoka nje,
“Serikali ya awamu ya sita inasimamia masuala ya usafi na tunapoongelea suala la usafi linatusaidia kujilinda na magonjwa ya mlipuko na uchafu wa mazingira ndio unaotusababishia maradhi mfano mtu akiumwa kipindu pindu moja kwa moja ni amekula kinyesi “ amesema Dk Magembe
Sambamba na hayo amesema kwa mkoa wa Dar es salaam umefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa kipindu pindu ugonjwa ambao uliokuwa ukilisumbua jiji hilo na ni kutokana na kutotunza mazingira.
“Jiji la Dar es salaam tulikuwa tuna misimu kila mwaka kuna wagonjwa ya kipindu pindu lakini sheria iliposimamiwa ya usafi wa mazingira mpaka sasa tuna miaka mitano hakuna rekodi ya wagonjwa wa kipindupindu”
Awali akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Masuala ya mazingira nchini, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya Mazingira na Usafi, Wizara ya Afya Dkt. Khalid Massa, amesema, kwa sasa hali ya watu kuwa na vyoo bora nchini imeongezeka kutoka asilimia 42 ya mwaka 2017 na kufikia asilimia asilimia 70 kwa mwaka 2021.
Dkt. Massa amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati waliojiwekea hivyo kupunguza kaya zisizo kuwa na vyoo kutoka asilimia 9.6 hadi kufikia asilimia 1.3 kwa mwaka 2021.
Vilevile amesema vyombo vya kunawia mikono kwenye kaya vimeongezeka kutoka asilimia 5.6 ya mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 41.7 kwa mwaka 2021, lakini pia wameendelea kuchukua hatua za kulinda mipaka kwa kuwaajiri na kuwapeleka vijana wapatao 70 kwa ajili ya masuala ya Afya Mazingira mipakani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maafisa Afya na Mazingira nchini Twaha Mubarak ameiomba Serikali, kuangalia utaratibu wa uteuzi wa Maafisa Afya hao, kwani kwa kipindi cha sasa hawaridhishwi na uteuzi wao kunafanywa na Mganga Mkuu wa Wilaya au wa Mkoa suala ambalo Dkt. Grace Magembe, aliyekuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo ameahidi kulifanyia kazi.
Mkutano Mkuu wa Mwaka
wa Maafisa Afya Mazingira wenye Kaulimbiu isemayo Uimarishaji wa huduma za Afya
Mazingira na usafi katika mapambano ya Uviko -19 unafanyika jijini Dodoma,
ukiwa na lengo la kujitathmini juu ya utendaji kazi wao na kuweka mikakati kwa
ajili ya mwaka ujao.
0 Comments