📌SAIDINA
MSANGI, WFM
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amekipongeza Chama cha
Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina, (Hazina
Sacoss) kwa kutekeleza agizo la Serikali la kushusha riba za mikopo kwa
wanachama wake kutoka asilimia 12 hadi asilimia 11 kwa mwaka.
Hayo yalielezwa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya uendelezaji wa Sekta ya
Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dionisia Mjema kwa niaba ya Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akifungua Mkutano Mkuu
wa nane wa Mwaka wa Hazina Saccos Ltd uliofanyika katika
ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
“Sacoss ni nyenzo muhimu ya kupambana na umasikini, kujenga uchumi wa
kaya kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla hivyo ni muhimu kuwa na sacoss
imara na endelevu ambayo inatatua changamoto za wanachama”, alisema Dkt.
Nchemba.
Alisema ili kufikia azma hiyo viongozi wa Hazina Sacoss wanapaswa
kuimarisha mifumo ya kuweka akiba, kununua hisa na kuongeza huduma bora
na zenye gharama nafuu zinazokidhi matakwa ya wanachama hasa kuwa na gharama
nafuu za mikopo.
Dkt. Nchemba aliwataka viongozi wa Saccos hiyo kuwa na mpango wa
kuongeza wanachama wapya, kuongeza akiba za hisa zao, kuwa wabunifu na kufanyia
kazi changamoto na maoni yanayotolewa na wanachama.
Aidha Dkt. Nchemba aliwaagiza viongozi wa hazina sacoss kufanya tathmini
sahihi ya miradi yao ukiwemo mradi wa Njedengwa juu ya uwezekano wa kupata
mwekezaji ili wanachama waweze kunufaika na miradi hiyo na kuokoa fedha ambayo
inaonekana imekaa muda mrefu kwenye ardhi bila uzalishaji.
Waziri Nchemba aliwapongeza viongozi wa hazina sacoss kwa kuunga mkono
Serikali kwa kuendeleza jiji la Dodoma kwa kuwapatia viwanja wanachama wake
katika maeneo ya Ihumwa ngaloni, Iyumbu, Nzuguni na Ihumwa Ilolo sehemu ambazo
zilikuwa mapori yasiyotumika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Hazina Sacoss Bw. Aliko Mwaiteleke
alisema kuwa mtaji wa chama umekua na kufikia kiasi cha Sh. bilioni 18
ambazo zinajumuisha akiba za wanachama na hisa na ameongeza kuwa kama Chama cha
ushirika wamejipanga kusimamia kikamilifu kuhakikisha watumishi wengi
wanajiunga na ushirika huu ili waweze kunufaika.
‘’Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Hazina kilianzishwa mwaka 1972
wakati huo kikiwa na wanachama mia moja (100), lakini mpaka sasa chama
kinahudumia wanachama takribani 5,624’’ Alisema Bw. Mwaiteleke.
Aida, Bw. Mwaiteleke aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa
kuimarisha usimamizi wa Taasisi za Fedha nchini kwa kuanzisha sheria Namba 10
ya mwaka 2018 ya huduma ndogo za Fedha pamoja na kanuni zake za mwaka 2019 kwa
ajili ya ustawi wa sekta ya fedha nchini.
Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Hazina Bw. Aliko Mwaiteleke (kulia) akiteta jambo na Katibu wa Bodi hiyo Bw. Festo Mwaipaja wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho |
Aliongeza kuwa Hazina Saccos imejipanga kuwa chama chenye mlengo wa
kutoa huduma kulingana na mahitaji na changamoto zinazowakabili wanachama ili
waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Chama chetu kinatarajia kuongeza kiwango cha kukopa hasa mikopo ya
dharura kwa wanachama wetu kutoka shilingi milioni mbili (2,000,000/-) mpaka
shilingi milioni tano (5,000,000/-)
Bw. Mwaitekele
Bw. Mwaiteleke alitoa rai kwa wanachama kuwa waadilifu katika urejeshaji
wa mikopo wanayochukua ili kuweza kukuza mfuko wa chama na kuwezesha wanachama
wengi zaidi kunufaika na huduma zinazotolewa na chama hicho.
Mkutano wa mwaka wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Hazina unafanyika kwa
siku mbili Jijini Dodoma ambao unahudhuriwa na wajumbe kutoka Mikoa mbalimbali
nchini wanaowakilisha wanachama zaidi ya 5,000 kutoka kwenye mafungu (votes)
282 Tanzania Bara.
(Picha na Kitengo cha Mawailiano Serikalini – WFM, Dodoma)
0 Comments