📌JOSEPHINE MAJURA, WFM, ARUSHA
SERIKALI imeupongeza
Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Wizara ya
Fedha na Mipango kwa kuwaandaa wataalam ambao wanakidhi vigezo na matakwa ya soko la ajira Kitaifa na
kimataifa kwa kuwa na Mitaala ambayo wanafunzi
wanajifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson wakati
wa mahafali ya 23 ya IAA yaliyohusisha wahitimu kutoka Kampasi ya Arusha, Dar
es Salaam na Babati yaliyofanyika jijini Arusha.
Nimefurahishwa sana na ongezeko la kozi katika ngazi zote, si ongezeko tu lakini zaidi mitaala yenu inaonesha ni wataalamu wa aina gani mnaozalisha kama Taasisi ya Elimu ya Juu mnatekeleza jukumu lenu la msingi la kutoa elimu kwa viwango ninawapongeza sana
Dkt. Tulia.
Alisema kuwa orodha
ya kozi mnazotoa chuoni nyingi ni zile zinazojibu mahitaji ya wakati kwa kuwa
zitatoa mchango mkubwa wa kutoa wataalam watakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali
katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Tulia aliongeza kuwa Serikali inawategemea katika suala la kufanya tafiti
zinazoweza kuleta mchango chanya katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
kupitia viashiria vya kisekta katika maendeleo ya rasilimali watu, mazingira
wezeshi ya biashara, masoko na uratibu na mapinduzi ya kidigitali.
Aidha alitoa rai
kwa wahitimu kuhakikisha wanatumia elimu waliyopata kupambana na umaskini kwa ngazi ya mtu
mmoja mmoja, jamii inayomzunguka na Taifa, hatimaye kuisaidia jamii yake kuleta
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa letu kwa ujumla.
“Ninaamini mtakapotoka hapa baadhi yenu
mtaajiriwa kwenye Taasisi za Umma; wengine mtaajiriwa kwenye sekta
binafsi; na wengine mtajiajiri wenyewe kwa kuwa najua mmeandaliwa kufanya kazi
katika mazingira yote yaani kuajiriwa na kujiajiri. Nawaomba mkawe waadilifu na
mkalitumikie Taifa lenu kwa akili na nguvu zenu zote mkitanguliza uzalendo
mbele”, aliongeza Dkt. Tulia.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu
Arusha, Dkt. Mwamini Tulli, alisema kuwa Chuo kinaendelea kufanya tafiti mbalimbali ili kujua
mahitaji ya Watanzania ili kiweze kuanzisha kozi mbalimbali zinazokidhi
mahitaji yao ili kuondoa adha wanayoipata Watanzania kwenda kutafuta hizo kozi
nje ya Nchi kwa gharama kubwa.
Dkt. Tulli, aliongeza kuwa kozi zinazotolewa Chuo hapo ni kwa ajili ya wazawa na wageni
kutoka nje ya Tanzania, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanatimiza vigezo
vilivyowekwa kwa kozi husika.
”Nitumie fursa hii
pia kuwakaribisha wazawa pamoja na wageni toka nchi mbalimbali
ambao mmefika hapa hii leo kwa ajili ya kuwashuhudia wapendwa wenu wakitunukiwa
vyeti katika ngazi mbalimbali kuja kusoma hapa IAA kuanzia ngazi ya Astashahada
hadi Shahada ya Uzamili. Karibuni Sana IAA”, alisema Dkt. Tulli.
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, akizungumza wakati wa mahafali ya 23 ya chuo hicho yaliyohusisha wahitimu kutoka Kampasi ya Arusha, Dar es Salaam na Babati yaliyofanyika jijini Arusha.
|
Naye Mkuu wa Chuo Prof. Eliamani Sedoyeka, alisema kuwa kuanzia Januari
mwakani Chuo kinatarajia kuanza kutoa Shahada ya Uzamivu yaani Phd kwa kushirikiana na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Prof. Sedoyeka
aliongeza kuwa Chuo kinatoa takribani kozi 17 kwa ngazi ya
Astashahada, kozi 17 ngazi ya Stashahada, kozi 18 ngazi ya Shahada na kozi 12
za Shahada ya Uzamili.
Chuo cha
Uhasibu Arusha (IAA) ni moja ya kati ya Vyuo sita vilivyopo chini ya Wizara ya
Fedha na Mipango, jumla ya wanafunzi 2,481 wametunukiwa vyeti katika ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada ya Uzamili wahitimu.
0 Comments