Ndugu wananchi nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, saa chache zijazo tunaadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika sasa Tanzania Bara. Umuhimu wa siku hii katika historia yetu ni wa kipekee, kwani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuliyonayo leo isingeweza kuzaliwa Aprili 26, 1964, kama kusingelitanguliwa na Uhuru wa Tanganyika na baadaye Mapinduzi ya Zanzibar. Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa chachu ya kufanikisha muungano adhimu, na kupelekea Taifa letu kuwa la amani na mshikamano.
Katika harakati za kutafuta Uhuru
Mwalimu Nyerere alikuwa na wenzake 16. Nao ni
Abdul Wahid Sykes
Abubakar Ilanga
Ally Sykes
Cathbert Oswald Milinga
Dossa Aziz
Gelmandus Pacha
Japhet Kirilo
John Rupia
Joseph Kimalando
Joseph Kasela-Bantu
Kisunguta Kabara
Lameck Makaranga
Patrick Kunambi
Saadan Abdul Kandoro
Suleiman Kitwara
Tewa Said Tewa
Ninasikitika kuwa wengi wa waasisi wetu
17 walioshiriki kupigania Uhuru wa Tanganyika wakiongozwa na Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hatuko nao leo, wametangulia mbele ya
haki. Hakika wangetamani sana kuiona siku ya leo.
Kwa mujibu wa takwimu zetu za idadi ya
watu, Watanzania 2,520,559, sawa na asilimia 4.3 ya Watanzania wote milioni 59
waliopo sasa, ndio waliokuwa wamezaliwa kabla ya Disemba 9, 1961. Sisi ambao
tumepata bahati ya kushuhudia siku ya Uhuru na kuadhimisha miaka 60 ya uhuru,
huenda tusipate bahati hii ya kuadhimisha makumi kama haya mengine.
Mafanikio mengi tumeyapata tangu kupata
uhuru wa nchi yetu, mafanikio hayo si tu yatahitahitaji muda mrefu kuyaelezea
bali pia kupata kurasa nyingi ili kuweza kuyaandika.
Mafanikio ya Miaka 60 ya Uhuru
1. Kufanikiwa kuulinda uhuru au uhuru
wetu na mipaka yake
2. Kujenga umoja wa kitaifa na
mshikamano uliozaa na kulea amani na utulivu tulionao
3. Kuimarisha uchumi wetu na kupunguza
umasikini kulikotuwezesha kutoka kwenye kundi la nchi maskini na kuingia kwenye
kundi la nchi za uchumi wa kati wa chini
4. Kuongeza upatikanaji na kuboresha
huduma za jamii kwa wananchi
5. Kujenga heshima ya nchi yetu na
ushawishi kikanda na kimataifa
6. Kuimarisha Demokrasia na Utawala wa
Sheria
Jeshi letu limekuwa na weledi katika
ulinzi wa mipaka yetu, katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wetu, hatujapoteza
eneo letu na ni fahari kwa kuwa na jeshi lenye utii na uzalendo kwa Taifa letu.
Kama lipo eneo ambalo tumefanikiwa zaidi
ni kuboresha maisha ya wananchi. Tumeweza kuongeza upatikanaji wa maji maeneo
mbalimbali ya mijini na vijijini.
Wastani wa pato kwa mtu kwa mwaka 1961
lilikuwa ni shilingi 776 na kwa mwaka 2020 ni shilingi 2,653,790. Jambo hili
linaongeza hadhi yetu machoni pa jumuiya ya kimataifa na kutuondolea unyonge.
Kutokana na kukua kwa Uchumi katika nchi
yetu Usafiri wa anga si suala la anasa wala starehe hivyo kufufuliwa au
kuimarishwa kwa shirika letu la ndege ATCL ni jambo la lazima. Tumeishanunua
ndege 12 na malipo ya ndege nyingine 5 yamekwishafanyika
Tanzania inakadiriwa kuwa na makabila
zaidi ya 120, lakini pamoja na tofauti zote hizo tumeweza kuwa na Taifa moja na
kuweza kuunganishwa na lugha ya Kiswahili. Si kitu rahisi.
Katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru,
tumeweza kufikia uchumi wa kati mapema hata kabla ya lengo la kufikia uchumi
huo mwaka 2025, hali hii inatuondolea unyonge kimataifa na kutuondolea
unyanyapaa.
Tumeweza kuunganisha mikoa kwa barabara
za lami, na kazi ya kuunganisha makao makuu ya wilaya kwa barabara inaendelea.
Wakati tunapata uhuru tulikuwa na meli 6
na sasa tuna meli 14 zinazofanya kazi katika Ziwa Nyasa, Victoria na
Tanganyika.
Wakati tunapata uhuru nchi yetu ilikuwa
inazalisha megawati za umeme 17.5 tu, lakini sasa tunazalisha megawati 1909,
huku tukiwa na matarajio ya kuongeza megawati nyingine 2,115 tutakapokamilisha
ujenzi wa Bwawa la Nyerere [JNHPP].
Wakati tunapata uhuru tulikuwa na walimu
wa shule za msingi 36 lakini sasa tuna walimu wa shule za msingi 281,728".
Tumerudisha fursa ya watoto watoro na
waliopata changamoto mbalimbali kurudi shule.
Tumepiga hatua kwenye eneo la elimu ya
juu kwani kwa sasa tuna vyuo vikuu 30, vya serikali 18 na 12 vya sekta binafsi
na vyuo vishiriki 17.
Kilicho dhahiri katika sekta ya afya, ni
ule uwezo wa kutoa huduma za kibingwa ambazo zamani hazikuwepo na tulikuwa
tukilazimika kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutumia fedha nyingi za
kigeni.
Umri wa kuishi kwa Watanzania
umeongezeka kutokana na uboreshaji na upatikanaji wa lishe na kuondoa udumavu,
wakati tunapata uhuru wastani wa umri wa kuishi kwa Watanzania ulikuwa ni miaka
37 na sasa ni miaka 67.
Tanzania imeendelea kuimarika, nguvu ya
kushawishi imeendelea kukua na kuaminika ikiwemo Watanzania kuongoza taasisi
mbalimbali za Kimataifa. Tulikuwa na balozi mbili tu mwaka 1961 na sasa tuna
balozi 44. Diplomasia yetu inapanuka na inaendelea kung’ara duniani.
Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi
tuna vyama vilivyosajiliwa 19 na 17 vinavyoomba usajili wa muda, na tumekuwa na
mfumo bora na imara wa kuweka viongozi madarakani ambao unaheshimiwa na
kuaminiwa.
Tumekuwa na mfumo imara wa utoaji haki
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kwa kuzingatia msingi wa kuwa
binadamu wote ni sawa na hakuna aliye juu ya sheria.
Tutunze mazingira yetu kwa uchungu
mkubwa ili turithishe kwa watoto na vizazi vyetu nchi ambayo ni ya neema kama
ilivyokuwa kwetu.
Dira yetu ya maendeleo kufikia 2025
inaelekea kumalizika ambapo tunatarajia kukua kwa uchumi kwa asilimia 8.
Tunapoangalia mbele tunakwenda kuandaa dira ya miaka 25 ijayo (2025-2050)
ambayo itaelekeza kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Ndugu wananchi, kabla sijamaliza ninayo
kila sababu ya kuwashukuru na kutambua mchango wa viongozi wetu ambao wao na
awamu walizoziongoza wametufikisha kwenye haya makubwa tunayoshuhudia leo.
Wale waliotangulia mbele ya Haki tuombe
mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, Amen. Daima tutawakumbuka
na kuenzi michango yao adhimu kwa Taifa hili
Tuna kila sababu yakujivunia maendeleo
tuliyoyapata katika kipindi cha miaka 60, hatujafikia kilele cha matamanio yetu
lakini tulipofika si haba.
Mafanikio tuliyoyapata kwa miaka 60
yamebebwa na utawala wa sheria na utawala bora. Tumekuwa na mfumo bora
unaoheshimiwa wa kuweka viongozi madarakani kupitia chaguzi zinazofanyika kila
baada ya miaka mitano
Tutembee kifua mbele na kujisifu, wala
tusijifuje na kujipa unyonge na kwa vyovyote vile kwani mambo tuliyoyafanikisha
kwa miaka 60 ni mengi na makubwa kuliko yale yaliyofanyika nchini wakati wa
ukoloni. Tusilinganishe tu kina tulichofikia, na tukasahau kutazama urefu wa
kina tulichoanzia.
Kwa maneno haya niwatakie tena kila la
kheri katika kusherekea Uhuru wa Tanzania Bara
Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza, Kazi
Iendelee
Asanteni Sana.
0 Comments