📌DENNIS GONDWE
WAWEKEZAJI wenye viwanda nchini wamealikwa kuwekeza
katika ujenzi wa viwanda katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuchangia
katika ukuzaji wa uchumi na ujenzi wa makao makuu ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mipango Miji katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alipokuwa akiwasilisha fursa za uwekezaji
zilizopo katika Jiji hilo kwenye Mkutano wa Mwaka wa Shirikisho la wenye Viwanda
Tanzania (CTI) uliofanyika katika hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam.
Masanja alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
inaunga mkono juhudi za serikali za ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini. “Katika
kuunga mkono juhudi hizo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliandaa Mpango Kabambe
wa miaka 20. Mpango huo umeainisha matumizi mbalimbali ya ardhi. Halmashauri
imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Leo tunaleta kwenu fursa ya
viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika eneo la viwanda Nala. Eneo la
Nala lipo jirana na barabara kuu ya Singida, umbali wa kilometa 20 kutoka
katikati ya mji” alisema Masanja.
Akiongelea umuhimu wa eneo la viwanda Nala, alilitaja
kuwa eneo hilo ni la kimkakati likiwa na miundombinu muhimu ya umeme wa msongo
mkubwa, barabara na maji ya kutosha. “Eneo lina viwanja kwa ajili ya viwanda
vikubwa, vya kati na vidogo. Eneo lina viwanja kwa ajili ya viwanda vya kufua
umeme wa upepo, viwanda vya matengenezo ya magari, viwanda vya dawa, viwanda
vya nguo na viwanda vya vyakula. Vingine ni viwanja kwa ajili ya viwanda vya chuma,
viwanda vya mbolea na viwanja kwa ajili ya biashara” alisema Masanja.
Kwa upande wa kiongozi wa timu ya kimkakati ya
Uwekezaji na Masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leonard Machunde alisema
kuwa eneo la viwanda Nala ni eneo la serikali chini ya Halmashauri ya Jiji la
Dodoma. “Uzuri wa eneo hili, muwekezaji hatakiwi kupitia kwa dalali bali
anakuja moja kwa moja ofisi ya Halmashauri ya Jiji kwa ajili ya kupata kiwanja.
Hivyo, atapata kiwanja kwa gharama halisi. Gharama ya kiwanja ni shilingi 5,000
kwa mita mraba” alisema Machunde.
Mchumi mwandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
aliwataarifu wajumbe wa mkutano mkuu wa mwaka wa CTI kuwa Nala ni eneo la
kimkakati na sahihi kuwekezaji wa ujenzi wa viwanda. “Ni vizuri kuchangamkia
fursa hii kuwekeza katika ujenzi wa viwanda katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi. Kadri unavyokuja mapema ndivyo
unavyonufaika mapema. Makao makuu ya nchi lazima yatunufaishe wote” alisema
Mchumi Msangi.
0 Comments