Na Saida Issa, Dodoma
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan amefunga mafunzo ya siku nne ya Makatibu wa Chama Cha Mapinduzi wa Mikoa na Wilaya nchini.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa CCM Itikadi na uenezi Shaka Hamdu Shaka mara baada ya Mwenyekiti wa CCM kufunga mafunzo hayo katika ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM Makao Makuu Jijini hapa.
Katibu huyo amesema utaratibu wa mafunzo ndani ya Chama Cha Mapinduzi utakuwa endelevu kutokana na umuhimu wake katika kukidhi mahitaji ya wakati na mabadiliko ya mwenendo wa siasa za dunia.
"Mafunzo ni nyenzo muhimu sana katika kuongeza weledi na ufanisi wa kufikia malengo ya taasisi yoyote ile, Chama Cha Mapinduzi tutafanya utaratibu huu kuwa endelevu ili kukidhi mahitaji ya wakati na mwenendo wa mabadiliko ya siasa za dunia,"amesema Shaka.
"Uongozi ni kushirikishana, uongozi ni kukumbushana mara kwa mara ili wote muende pamoja. Njia hii ni muhimu kwa watendaji wetu kwani inawaongezea uwezo wa kufikiri na kutenda siku hadi siku," amefafanua.
Aidha Katibu huyo amehimiza umoja, mshikamano na maelewano miongoni mwa viongozi na wanachama wa CCM ili kazi ya kuendelea kukiimarisha chama katika kuwatumikia wananchi iwe ni endelevu na ya kudumu hatimaye ilete tija ikizingatiwa kuwa Chama Cha Mapinduzi kimebeba matumaini makubwa ya watanzania katika kuwaletea maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mafunzo yalilenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji, uweledi na ufanisi watendaji wa Chama Cha Mapinduzi wa Mikoa na Wilaya katika kusimamia katiba ya CCM, kanuni, ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025, maelekezo ya vikao na masuala mbalimbali ya kuisimamia serikali na ujenzi wa Taifa.
0 Comments