Na Zainabu Mtoi,
SHEIKH wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu amewataka waumini ndani ya nyumba za ibada kuhakikisha wanawatii viongozi waliopo madarakani wakiwemo wakidini na wakiserikali.
Akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu kwenye Msikiti wa Paranga wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, shekh.Mustapha amesema waumini wakiwa na tabia ya kujenga nidhamu wataweza kudumisha amani ambayo ni tunu waliyopewa na Mwenyezi Mungu na itaondoa migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza ndani ya nyumba za ibada.
“Mkumbuke kuwa hata Mtume (S.A.W) alikuwa na tabia nzuri,hivyo tunatakiwa kuifuta kwa vitendo,hivyo nidhamu ikiwepo italinda amani na itaondoa vurugu za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa baadhi ya nyumba za ibada”amesema.
Aidha amewataka waumini kuhakikisha pia wanajihadhali kwa kuchukua hatua ya kujilinda juu ya ugonjwa wa corona bila kupuuzia huku wakifuaata maelekezo ya wataalamu wa afya pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali wanaoelimisha juu ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa bado kuna ugonjwa hivyo watanzania hawapaswi kuzembea na wanatakiwa kuendelea kujihadhali na kuchukua tahadhali dhidi ya Uviko -19 ili wasiweze kuambukizwa.
Aidha kwa upande wake Bakwata wilaya ya Dodoma imewapongeza umoja wa wanawake wa kata ya Chang’ombe (WASTARA) wakiwemo na wadau mbalimbali kwa kuweza kuchangia shughuli za kimaendeleo zinazoendeshwa kidini na kijamii.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bakwata wilaya ya Dodoma Bashiru Omary kwa niaba ya Baraza kuu la waislamu Tanzania wilaya ya Dodoma,baada ya kupokea vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya milioni 4.4 ikiwemo nondo na mifuko ya simenti vilivyotolewa kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa kisasa wa Muccadam uliopo Kata ya Chang’ombe.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa Bakwata wilaya inawapongea wanawake hao wa kata ya hiyo kwa kutoa michango mbalimbali ya kidini na kijamii wakiwemo pia na wadau wa maendeleo ambao wanaoendelea kutoa misaada yao ya kifedha,mali na nguvu kazi.
Omary amesema kwa upande wa umoja wa wanawake wameweza kuchangia ujenzi wa msikiti huo kwa kutoa mifuko 11 ya simenti ikiwemo na kujitolea nguvu kazi zao ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
MWISHO.
0 Comments