WAKULIMA 22,000 WANUFAIKA SOKO LA MTAMA KUPITIA WFP

 

NA MUSSA YUSUPH

DODOMA

SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ilimewaunganisha wakulima 22, 000 kutoka wilaya tano za mkoa wa Dodoma, kwa wanunuzi wa mtama nchini Sudan Kusini baada ya kuwepo mahitaji makubwa ya zao hilo.


Akizungumza jijini hapa na waandishi wa habari, Mkuu wa Ofisi Ndogo ya WFP, Neema Nima Sitta, alisema wakulima hao wameuza tani 17,000 ya zao hilo zilizowaingizia zaidi ya sh. bilioni tisa kwa miaka miwili pekee.


Alisema wakulima walionufaika kupitia mpango huo ni kutoka wilaya za Dodoma, Kondoa, Chemba, Mpwapwa, Bahi na Dodoma.


“Wakulima hao wamenufaika kupitia mradi wa WFP wa kilimo himilivu cha mtama unaoendeshwa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Zao la mtama lina soko kubwa Sudan Kusini, hivyo WFP inaendesha programu maalum ya kulima zao hilo katika vijiji zaidi ya 200 vya wilaya za mkoa wa Dodoma,” Neema, alieleza.


Alibainisha kuwa WFP linawatafutia soko wakulima hao kwa mashirika binafsi katika nchi hiyo huku WFP likiwa sehemu ya wanunuzi kwa ajili ya matumizi katika kambi za wakimbizi.


Neema alieleza kuwa katika mradi huo ambao WFP inashirikiana na serikali, umeanza na vijiji 203 katika Mkoa wa Dodoma na lengo ni kupanua mradi huo kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya mtama Sudan kusini.


Alisema mtama wa Tanzania ambao unapata soko kubwa nchini Sudan Kusini unalimwa kwa kuzingatia kanuni za kilimo hai kwa kuondoa matumizi ya mbolea za viwandani na dawa.


“WFP kama wadau muhimu kwa kushirikiana na serikali, tunajivunia mradi huu ambao umekuwa na mafanikio makubwa, tumegundua zao hilo limekuwa hitaji kubwa kwa nchi ya Sudan Kusini.


Aliongeza kuwa: “Kutokana na uhitaji huo mkubwa wa soko la mtama, WFP wanafikiria kupanua mradi huo na kufikisha katika wilaya nyingi na mikoa mingine ya Tanzania.”

Post a Comment

0 Comments