VIJANA WAASWA KUTUMIA FURSA YA UKUAJI WA TEKNOLOJIA KATIKA UBUNIFU WA VITU.


 

Na,Saida Issa-Dodoma

VIJANA nchini wametakiwa kutumia fursa ya ukuaji wa teknolojia duniani kubuni vitu vitakavyo wawezesha kujiajiri ili kukabiliana na tishio la mashine kuchukua ajira zinazo fanywa na binadamu.

Mkurugenzi mkazi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Girl Effect, Dolorosa Duncan alibainisha hayo juzi kwenye mjadala kuhusu mchango wa vijana katika maendeleo ya nchi ulioandaliwa na Asasi za kiraia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Azaki.

Duncan, alisema vijana wanatakiwa kutumia fursa ya ukuaji wa teknolojia duniani kubuni vitu mbalimbali vya kujipatia ajira ili kukabiliana na changamoto hiyo.

“Ukuaji wa teknolojia una changamoto zake lake pia una fursa ambazo sisi kama vijana tukizitumia vizuri tunaweza kukabilaina na changamoto ya ukosefu wa ajira duniani”alisema Duncan

Vilevile, alisema hivi sasa duniani lipo tishio la baadhi ya ajira kuchukuliwa na mashine kutokana na ukuaji wa teknolojia hivyo vijana hawanabudi kujiandaa na changamoto hiyo.

Kadhalika alisema kupitia teknolojia zipo fursa nyingi za ajira ambazo vijana kama watazitumia vizuri zinaweza kuwatoa kimaisha na kuacha kuendelea kulalamika.

Pia, alitoa wito kwa viongozi mbalimbali katika sekta binafsi pamoja na serikalini kuwaamini vijana na kuwapa nafasi ili wajifunze.

“Tunatakiwa kuwaamini vijana hata vijana waliofanikiwa kuna watu ambao waliwaamini wakawaacha wakose lakini leo hii wamekuwa viongozi wazuri katika nafasi mbalimbali”alisisitiza

Aidha, Mkurugenzi mtendaji wa The Foundation for Civil Society Francis Kiwanga, alisema kuwa siri kubwa ya vijana kukuwa ni kufanya kazi zao vizuri.

“Kijana fanya kazi yako vizuri watu wataona tuu hii ndiyo siri kubwa ya kupata mafanikio hata kama uko wapi lakini kazi yako nzuri itakutambulisha lakini pia niwaambie kama unafanya kitu fanya usiogepe kwani neno hili limeandikwa kwenye biblia zaidi ya mara 365 hivyo vijana tusiogope”alisema Kiwanga

Afisa mtendaji mkuu wa shirika la Legal services facility (LSF) Lulu Ng’wanakilala alisema vijana wanapaswa kuaminiwa katika nafasi mbalimbali bila kujali umri wao.

“Mimi katika ofisi yangu ndiye mzee wote ni vijana na ninawaamini kwasababu ninachoangalia ni uwezo na siyo umri kwani vijana wanaweza kufanya mambo kama vile mtu mwingine anavyoweza kufanya kikubwa tunapaswa kuwapa nafasi”alisema

Mwisho

Post a Comment

0 Comments