VYOMBO VYA HABARI VYAUNGANA KUFANYA KAMPENI YA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU.


 Na Agness Peter, Zainabu Mtoi, Josephine Mtweve,

SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na makampuni ya Clouds Media Group, Wasafi Media na Mwananchi Media Group wameweka ushirikiano katika kuadhimisha miaka 60 ya uhuru ili kutambua mchango wa wananchi na viongozi katika kazi kubwa ya kuleta uhuru na kuhamasisha dhana ya uzalendo.

Akizungumza na  waandishi wa habari katika uzinduzi wa kampeni ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru jijini Dar-es-salaam Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, Gabriel Nderumaki amesema ushirikiano huo ni matunda ya kuwa pamoja na katika kuangalia muktadha wa nchi.

Amesema lengo ni kuwaunganisha watanzania katika maadhimisho hayo na kutumia changamoto na fursa walizozipata kwa Taifa kwa ajili ya kutengeneza mustakabali utakaoleta tija  kwa watanzania pamoja na kuwakumbusha vijana kuhusu walipotoka, walipo na wanapokwenda.

‘’TBC kama chombo cha utangazaji cha umma kina dhima ya kuleta umoja kwa watanzania na pia kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali yetu chini ya mheshimiwa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania  hivyo ushirikiano huu utawezesha wananchi kufika ndani na nje ya nchi yetu,’’ amesema.

Aidha Mkurugenzi mkuu wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga amesema vijana wengi kwa sasa hawajui mambo mengi ambayo taifa limewafanyia lakini taifa lina mambo mengi ya wao kujifunza hivyo vizazi vya sasa vinatakiwa kujua historia na mambo mengi kuhusu taifa lao.

Amesema wao kama chombo cha habari cha vijana wanatakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba wanashirikiana na kuweza kuungana katika kutekeleza jambo la kuwaelimisha watanzania na  ni historia katika taifa kuhakikisha vyombo vya habari vinaungana na vinakuwa kitu kimoja.

‘’Wengine sisi tuliweza hata kusafiri kwenda  sehemu nyingine unashangaa kuona kwamba hii nchi ina uzuri wa kiasi gani ambapo vijana wengi hawajui wengine wanafikiria kwamba holidays ni kwenda nje ya nchi ya Tanzania lakini holiday kubwa inaweza kufanyika katika nchi yetu, ‘’ amesema Kusaga.

Kampeni ya madhimisho hayo itasaidia kukuza utamaduni na mila ndani ya miaka 60 ya uhuru kutokana na mmomonyoko wa maadili kwa vijana. 

Post a Comment

0 Comments