Na Agness Peter,
SERIKALI imezitaka Taasisi za sekta binafsi pamoja na makampuni yanayojishughulisha na mawasiliano kushirikiana na Serikali kuhakikisha malengo ya serikali ya kufikisha huduma za intaneti kwa asilimia 80 vijijini yanatimia kwa haraka.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akifungua warsha ya mafunzo ya uchumi wa kidigitali yaliyoandaliwa na kampuni ya simu ya HUAWEI jijini Dodoma, Katibu Mkuu wizara ya habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Zainabu Chaula amesema lengo la serikali ni kuboresha huduma ya mawasiliano vijijini.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kujifunza TEHAMA ambayo inawezesha wananchi na uchumi kukua kidigitali hasa kwa watumishi wa Serikali katika matumizi sahihi ya TEHAMA na katika kujifunzia mambo ya utafiti katika sekta mbalimbali za ukuaji wa uchumi.
"Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM inasema tutafikisha intaneti vijijini karibu asilimia 80 wenzetu HUWAWEI wana Teknolojia lakini hatukuwaita tu HUWAWEI tumewakaribisha taasisi , sekta binafsi na makampuni yoyote yenye teknolojia rahisi ya kutufikisha huko tutafanya nao kazi kwa karibu," amesema.
Aidha amesema anaimani katika kila mwaka wataongeza wadau ili ifikapo mwaka 2024/25 wawe wamefikisha asilimia 80 na si vibaya wakiwafikia watanzania wote.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Mchumi mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Shadrack Muhagama amesema kuwa mafunzo hayo ya kidigitali yatawasaidia kuleta maendeleo hususani katika masuala ya kibiashara.
Amesema kwa nchi ya Tanzania wanashughulikia masuala ya uchumi lakini masuala ya kidigitali yanaenda kwa kasi sana hivyo hawawezi kujitenga nayo hivyo wanatakiwa wawe sehemu mojawapo ya uchumi wa kidigitali.
"Kwenye maisha ya vijijini Mtandao ni changamoto sana lakini ndipo wanakozalisha mali katika mafunzo haya mategemeo yangu tutaangalia approach namna gani tunaweza kuwafikia watu wa vijijini na wenyewe waweze kuchangia katika uchumi wa taifa hili kwa kutumia mtandao," amesema.
Pia Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya HUAWEI Nchini Tanzania, Tom Tao amewataka wakulima hapa nchni kutumia fursa ya mawasiliano ya kidigitali katika kuuza mazao yao kwenye masoko ya juu.
0 Comments