MAAFISA NA MAASKARI TAWA WATAKIWA KUTUNZA NIDHAMU NA KUWA MFANO KWA WANANCHI.

                                                                          


 Na Josephine Mtweve,

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi  Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) Meja Jenerali Mstaafu Hamisi Semfuko, ametoa rai kwa maafisa na maaskari wa Mamlaka hiyo kutunza nidhamu na kuwa mfano kwa wananchi wengine.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya uhifadhi kanda ya kati na kuvisha vyeo maafisa na askari wa uhifadhi wilayani manyoni Mej.Jenerali Semfuko amesema Askari ni watu wa kutegemewa hivyo wanatakiwa kutunza nidhamu ya hali ya juu na kuhakikisha  wanakuwa mfano kwa wananchi wengine.

Amesema kazi ya Askari ni kuwa mtumishi wa watu na si kunyanyasa wananchi bila sababu pia hivyo hatopenda kusikia Askari au Maafisa wa TAWA ndio watu wanaofanya fujo mjini.

‘’Sisi ni kioo cha jeshi lote la TAWA kokote kule tuliko kwahiyo tutunze nidhamu na kwa sasa  sheria ambazo tumeziweka na ambazo ziko karibu kutekelezwa zitakua ni kali na za haraka na hazina kamati ya nidhamu, mkuu wa kambi anatoa adhabu hapohapo na adhabu zetu zinazotolewa kwasababu zipo katika sheria za nchi anaweza kukufunga hata magereza,’’amesema.

Aidha mej.Jenerali Semfuko amesema jengo lililofunguliwa ni mwanzo wa miradi mingine ambayo itatekelezwa katika maeneo hayo, ambapo Bodi imeadhimia katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kuweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa malazi ya Askari 

Amesema Askari wanatakiwa kuishi ndani ya hifadhi ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri na kutunza nidhamu nzuri, pia wakikaa pamoja katika kambi wataweza kutatua matatizo yanayotokea na kulinda maisha na mali za wanachi wakati wanyama waharibifu watakapotokea katika maeneo hayo.

‘’ Kutakua na ujenzi mkubwa ambao utawapa fursa wananchi kwasababu matofali yananunuliwa hapahapa mabati yananunuliwa hapahapa pamoja na mafundi wengi wanatoka hapahapa kwahiyo tutahakikisha tunatumia nguvu za wajenzi zilizopo katika maeneo ambayo tunajenga na si kutoka maeneo mengine,’’amesema.

Kwa upande mwingine Mej.Jenerali Semfuko amesema kuna utaratibu ambao utaanza karibuni watanunua gari la kwanza la kuchimba visima vya maji pamoja na kununua helicopter kwaajili ya kufika kwa wakati sehemu husika ambapo wataweza kuwadhibiti wanyama wa haribifu kwa kutumia teknolojia.

Naye kamishna wa TAWA Mabula Nyanda amesema katika kipindi cha  mwaka 2021/22 bodi imetenga fedha jumla ya shilingi bilioni 19.9 kwaajili ya ununuzi wa mitambo na kutekeleza miradi ya ujenzi hususani miundombinu kwaajili ya utawala na utalii ambao baadhi yake utafanyika kanda ya kati.

Kamishna Nyanda amesema zoezi la kuvishwa vyeo maafisa 14 na askari wa hifadhi 6 limefanyika ikiwa ni utekelezaji wa taratibu za kijeshi na kuwakumbusha maaskari waliotunukiwa vyeo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwaongoza vyema watumishi wanaowasimamia.

Post a Comment

0 Comments