Na Agness Peter, Josephine Mtweve, Zainabu Mtoi,
WAFANYABIASHARA wa soko kuu la Majengo Dodoma wameuomba uongozi wa soko pamoja na uongozi wa jiji kutanua mifereji ya kupitisha uchafu na kutengeneza chemba zinazomwaga maji taka ili kuepukana na harufu mbaya katika eneo la soko hilo.
Akizungumza katika eneo la soko leo jijini Dodoma, Balozi wa eneo la Block D sokoni hapo Msafiri Mohamed amesema uchafuzi wa chemba na mifereji katika soko hilo ni kero kubwa kwa sababu miundombinu ya utiririkaji wa maji si rafiki kwa watu.
Amesema mifereji na chemba zinaziba na huwa inachukua muda mrefu mpaka kuja kuzibuliwa na kusafishwa hivyo inasababisha harufu kali kwa wanunuzi pamoja na wafanyabiashara wa soko hilo.
‘’Kwa mfano maji tiririka yanayotoka Buchani huenda moja kwa moja kwenye mifereji yanachukua muda mrefu na usafishaji unakuwa na harufu kali, harufu hii inatubugudhi sisi wafanyabiashara pamoja na wateja wetu katika soko la majengo,’’alisema.
Mmoja wa wafanyabiashara katika soko la majengo, Richard Jacob amesema wamelazimika kuizoea hali hiyo kwani wamekwisha peleka malalamiko kwa uongozi wa soko hilo lakini hayajafanyiwa kazi.
Ameongeza kuwa msimamizi wa soko hilo hasimamii vizuri kwa sababu anashindwa kukemea watu wanaopeleka takataka za mifuko ya samaki, takataka za Buchani na maji machafu katika eneo hilo matokeo yake hali ya mazingira yanakuwa machafu kwa usimamizi mbovu.
‘’Natoa ushauri kwa wasimamizi wa mazingira wa eneo hili wabadilishwe labda inaweza kuleta mabadiliko lakini kwa waliopo wamekuwa na mazoea sana,hivyo wanachukulia kuwepo kwa uchafu katika maeneo haya ni jambo la kawaida tu.Alisema
Aidha Kharifa Omari amesema changamoto kubwa ni katika kipindi cha mvua mifereji inaziba na kushindwa kupitisha maji hivyo serikali ifanye utaratibu wa kuwatoa watu wenye vibanda vilivyo juu ya mifereji ili usafi uwe rahisi kufanyika.
0 Comments