Ofisi ya Makamu wa Rais imesaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 18.8 na Kampuni
ya ujenzi ya SUMA JKT wa kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu
wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi huo imefanyika katika Ofisi ya Makamu wa
Rais Mtumba jijini Dodoma Oktoba 13, 2021 na kukabidhi rasmi eneo la ujenzi
kwa Mkandarasi baada ya kushinda zabuni, na kushuhudiwa na Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) ambaye ndio Msimamizi Elekezi wa ujenzi wa jengo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary
Maganga ameipongeza SUMA JKT kwa kushinda kandarasi hiyo na kutaka
ujenzi uwe wa haraka kwa kuzingatia ubora, viwango na kasi.
“Ninaamini kuwa SUMA JKT mna uzoefu mkubwa, na ujenzi huu utaenda kwa
kasi, na kuzingatia viwango vya ubora wa hali ya juu, na ikiwezekana mkamilishe
kazi hii kabla ya muda uliopangwa,” amesema Bi. Mary Maganga.
Aidha, Katibu Mkuu alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza ufanisi katika
utekelezaji wa majukumu kwa kuwa Serikali ilipohamia Dodoma jengo
lililojengwa katika eneo la Mtumba halitoshelezi mahitaji ya watumishi wote hivyo
kulazimika kutumia jengo lingine mjini kwa ajili ya watumishi wa idara zingine.
“Wenzetu wa Idara ya Mazingira wapo wengi na wana majukumu mengi kila
tunapowahitaji kuja kwa ajili vikao inabidi waje huku Mtumba kwa hiyo jengo hili
likikamilika ndani ya muda tuna imani ufanisi utaongezeka na tunaweza kufanya
kazi kwa pamoja na muda tunaotumia barabarani utapungua au kuondoka
kabisa,” alisema.
Aidha, Bi. Mary Maganga amesema, msimamizi wa ujenzi huo Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) atafanya kazi kwa karibu na Kamati ya Ujenzi ya Ofisi ya Makamu
wa Rais inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Mohammed Khamis Abdullah
na kusisitiza kutenga Ofisi kwa ajili ya Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
“Ofisi ya Makamu wa Rais ndio wasimamizi wa Masuala ya Muungano na
Mazingira hapa nchini, hivyo tutatoa nafasi katika jengo hili jipya kwa ajijli ya
wenzetu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali kwa upande wa Zanzibar
kupata nafasi ili kurahisisha masuala ya uratibu wa utekelezaji wa majukumu ya
Serikali kwa pande zote mbili za Muungano.” ameongeza Bi. Mary Maganga.
Naye, Mhandisi Morgan Nyonyi kutoka SUMA JKT amemthibitishia Bi. Mary
Maganga kuwa, SUMA JKT watatekeleza mradi huo kwa ustadi mkubwa kwa
kuhakikisha wanakailisha mradi huo wa ujenzi kwa wakati na ikiwezekana kabla
ya miezi 24 iliyopo ndani ya Mkataba.
“Tutajitahidi kwenda na wakati na kuzingatia viwango vya ubora, rasilimali fedha
na rasilimali watu tunao wa kutosha. Naishukuru Serikali kwa kutoa kiasi kikubwa
cha fedha zitakazowezesha kutekelezwa kwa mradi huu na Ofisi ya Makamu wa
Rais kwa kutuamini SUMA JKT” Alisisitiza Mhandisi Nyonyi.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Kihandisi wa NHC, Mhandisi Manning
Mwalaka, amesema Shirika litahakikisha Mkandarasi anafuata taratibu zote za
ujenzi kwa mujibu wa mkataba katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.
“Sisi na NHC tumepewa dhamana ya kuwa wasimamizi katika mradi huu,
tutashirikiana kwa pamoja, na kuhakikisha kwamba hili jengo linajengwa kwa
viwango vilivyokusudiwa,” ameeleza Mhandisi Mwalaka.
Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, kutapelekea Idara na Vitengo vyote vya
Ofisi ya Makamu wa Rais kuhamia katika jengo hilo.
0 Comments